Mzee Moi alazwa Hospitali ya Nairobi

Muktasari:

  • Taarifa za Moi kulazwa zilitolewa na ofisi yake. Moi alifikisha umri wa miaka 94 Septemba na sherehe fupi ilifanyika nyumbani kwake Kabarak katika Kaunti ya Nakuru.
  • Taarifa iliyotolewa na katibu wake Lee Njiru ilisema alikuwa na watu wa karibu katika familia ambao ni pamoja na watoto wake na wajukuu.
  • Moi, aliyetawala Kenya kuanzia mwaka 1978 hadi 2002, Machi mwaka huu alikwenda Tel Aviv, Israel ambako alifanyiwa uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Ichilov.
  •  “Mzee amepewa ruhusa baada ya madaktari kuridhishwa na maendeleo ya afya yake kufuatia uchunguzi wa goti lake, ambalo lilikuwa likimsumbua na kumkosesha furaha,” ilisema taarifa kutoka ofisi yake.

Nairobi, Kenya. Rais wa zamani Daniel arap Moi Jumatano mchana alilazwa katika Hospitali ya Nairobi kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida vya afya yake.
Hata hivyo, tabibu wake Dk David Silverstein alisema atabaki hospitalini hapo kwa siku kadhaa ili madaktari waweze kupata muda wa kutosha kufuatilia afya yake.
Taarifa za Moi kulazwa zilitolewa na ofisi yake. Moi alifikisha umri wa miaka 94 Septemba na sherehe fupi ilifanyika nyumbani kwake Kabarak katika Kaunti ya Nakuru.
Taarifa iliyotolewa na katibu wake Lee Njiru ilisema alikuwa na watu wa karibu katika familia ambao ni pamoja na watoto wake na wajukuu.
Moi, aliyetawala Kenya kuanzia mwaka 1978 hadi 2002, Machi mwaka huu alikwenda Tel Aviv, Israel ambako alifanyiwa uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Ichilov.
Alipokuwa Israel alipata fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika jiji la Jerusalem.
“Mzee amepewa ruhusa baada ya madaktari kuridhishwa na maendeleo ya afya yake kufuatia uchunguzi wa goti lake, ambalo lilikuwa likimsumbua na kumkosesha furaha,” ilisema taarifa kutoka ofisi yake.
Ofisi ya Moi iliwahi kukanusha madai kwenye mitandao ya kijamii kuhusu afya yake. Goti lilianza kumsumbua Julai 30, 2006 kutokana na ajali aliyopata mjini Limuru. Alikuwa akirudi
Kabarak akitokea Machakos, ambako alikuwa ameongoza sherehe za mahafali katika Chuo cha Thiolojia cha Scotts.
Januari 27, 2017 rais huyo wa zamani alifanyiwa operesheni ndogo ya goti katika Chuo Kikuu cha Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.