Dk Mndolwa aitaja mikakati ya ushindi CCM 2020

Muktasari:

Vuguvugu la Uchaguzi Mkuu limewaibua Jumuiya ya Wazazi (CCM) na kuweka bayana mikakati wanayoitumia kuhakikisha wanashinda chaguzi zijazo ndani ya chama hicho.


Dar es Salaam. Wakati joto la Uchaguzi Mkuu likiendelea kupamba moto ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho imesuka mikakati yake ili kuhakikisha chama hicho tawala kinabakia madarakani.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk Edmund Mndolwa ametaja mikakati minne itakayowawezesha CCM kushinda chaguzi zijazo ikiwamo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza leo, Desemba 15, 2018 na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya jumuiya hiyo tangu alipochaguliwa Desemba, mwaka jana alisema mipango hiyo ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama wapya.

Mapema mwakani utafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Hata hivyo ndani ya CCM kumeibuka vuta nikuvute katika nafasi ya urais huku ikidaiwa kuwapo kwa makundi ambayo yameanza kuandaa watu wao kwa ajili ya urais.

Dk Mndolwa amesema mpango uliopo ni kuongeza idadi ya wanachama kwani ndiyo mtaji mkuu katika chaguzi hizo.

"Nasikia saa hizi tuko karibu 12 milioni katika uchaguzi wa mwaka 2015 tulikuwa kama milioni nane, tumeshaongeza wanachama wengi sana kwa sababu ni mtaji wa kushinda uchaguzi," amesema.

Pia amesema watahakikisha ilani ya chama hicho inatekelezwa kwa kiwango cha juu ili yale waliyoahidi katika kampeni za mwaka 2015 yaweze kutekelezeka kabla ya kufika mwaka 2020.

Dk Mndolwa amemsifu Rais John Magufuli kuwa ni mtekelezaji mkuu wa ilani hiyo na anafanya vizuri kutokana na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

"Tunahakikisha ilani ya uchaguzi inatekelezwa kwenye ngazi ya kata, wilaya na mkoa," amesema.

Ameutaja mkakati mwingine kuwa ni kuhakikisha viongozi wa chama hicho wanasikiliza kero za wananchi na kuzitolea ufumbuzi ili kujenga imani kwa wapiga kura wao.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema kuwa ndani ya chama hicho hakuna matumizi  makubwa ya rushwa kama wengi wanavyodai, bali ni kutokana na mipango mizuri inayowavutia wanachama wapya wakiwamo kutoka vyama vya upinzani.