2018 ulikuwa mwaka wa mapigo kwa wapinzani

Muktasari:

  • Matukio mbalimbali ya kisiasa yaliyotokea katika mwaka huu unaoelekea ukingoni yaliwatesa wapinzani, baadhi yao wakiwa na kesi mahakamani


 

Mwaka 2018 unaelekea ukingoni huku ukiacha kumbukumbu ya matukio makubwa ya kisiasa. Hamahama za wabunge na madiwani wa upinzani kwenda CCM, kusomwa bungeni kwa muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa na mvutano wa kidiplomasia kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ni machache tu kati ya hayo.

Wabunge, madiwani upinzani watimkia CCM

Mwaka huu hautasahaulika kirahisi kwa vyama vya upinzani kutokana na wimbi la wabunge, madiwani na makada wake kuhamia CCM wakidai kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na Rais John Magufuli.

Zaidi ya madiwani 146 na wabunge 10 wa upinzani wametimkia CCM mwaka huu, huku chama kikuu cha upinzani, Chadema kikiathirika kwa kupoteza madiwani 137 na Chama cha Wananchi (CUF) wakifikia tisa.

Aliyefungua mwaka kwa kuhama upinzani alikuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) ambaye alitangaza kujivua ubunge na kuhamia CCM Desemba 2, 2017, akifuatiwa na Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) Desemba 14.

Baada ya kuvihama vyama vyao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi wa marudio Februari 17, 2018 na wabunge hao walipitishwa tena na CCM na wakashinda.

Kuanzia hapo mchezo wa hamahama ukaendelea, ukifuatiwa na wabunge wa Monduli, Julius Kalanga, Mwita Waitara (Ukonga), Pauline Gekul (Babati Mjini), James Ole Millya (Simanjiro) wote wa Chadema, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiwapoteza pia Zuberi Mohamed (Liwale) na Abdallah Mtolea (Temeke).

Wakati hamahama hiyo ikiendelea, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Tumezingatia na tumeweka jitihada zetu zote katika kushughulikia shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndiyo mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao kujiunga na CCM. Watakaoikosa round (zamu) hii mbaki hukohuko tutakutana 2020.”

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro naye alikiacha chama hicho Agosti 11 na kujiunga na CCM.

Matumaini ya Katiba Mpya

Tukio jingine kubwa la kisiasa ni pale, Rais John Magufuli alipotamka Oktoba 31 kuwa Serikali yake haipo tayari kutoa fedha za kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya.

Kauli hiyo iliwaamsha wadau wa Katiba na haki za binadamu waliopinga msimamo huo wakisema madai ya Katiba siyo utashi wake, bali ni matakwa ya wananchi.

Akizungumza katika kongamano la siasa na uchumi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema licha ya kufahamu hamu ya Watanzania kuwa na Katiba Mpya, anashindwa kuelewa kama ili kuipata katiba hiyo mchakato wake utatakiwa uanzie kwenye Katiba Inayopendekezwa au rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Rais Magufuli aliwahi kutoa kauli kama hiyo Novemba 4, 2016 alipozungumza na wahariri Ikulu Dar es Salaam, akisema hakuwahi kuahidi suala hilo kwenye kampeni, bali anataka kwanza kutekeleza ahadi alizowaahidi wananchi.

Dk Bashiru aula CCM

Miongoni mwa matukio yaliyovuma kisiasa mwaka huu ni kuteuliwa kwa Dk Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Mei 30, akimrithi, Abdulrahman Kinana aliyeomba kustaafu baada ya kuitumikia nafasi hiyo kwa miaka saba.

Uteuzi wa Dk Bashiru ulifanywa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli na kuthibitishwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho katika kikao chake kilichoketi Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuteuliwa, Dk Bashiru aliyekuwa mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipewa kazi ya kuongoza kamati maalumu ya kuhakiki mali za chama hicho.

Wapinzani wapinga muswada Sheria ya Vyama vya Siasa

Mwaka 2018 unakwisha huku vyama vya siasa vya upinzani vikijizatiti kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa vikidai kuwa una vipengele vyenye nia ya kuirudisha Tanzania kwenye mfumo wa utawala wa chama kimoja.

Vyama 15 vya upinzani vilikutana jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kuupinga muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni mjini Dodoma Novemba 16, 2018.

Kama hiyo haitoshi, vyama sita kati ya hivyo vilikutana Zanzibar Desemba 16 - 18 kutafakari hatima ya demokrasia nchini na vilitangaza kwamba 2019 ni mwaka wa kudai demokrasia.

Membe aitwa CCM kujieleza

Mzozo kati ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe nao ni tukio lililotamba mwaka 2018.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho mkoani Geita, Dk Bashiru alidai kuwa Membe anatuhumiwa kuandaa mipango ya kumkwamisha Dk Magufuli katika uchaguzi wa Rais na kwamba tangu ateuliwe kuwa katibu mkuu wa CCM hajawahi kuonana naye.

“Kati ya wagombea wote (wa urais mwaka 2015) wa CCM ni Membe peke yake ambaye sijakutana naye. Namkaribisha ofisini, aje anieleze ninayoyasikia ni kweli au si kweli,” alisema Dk Bashiru.

Kuitwa kwa Membe kuliibua vita mpya, baada ya ile ya kupambana na wasaliti wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambayo ilishuhudia makada wengine wakitimuliwa ndani ya chama hicho na wengine kupewa onyo.

Maazimio ya EU kwa Tanzania

Mwaka huu pia umeshuhudia kutetereka kwa uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) baada ya jumuiya hiyo kudai kuwa Balozi wake aliyekuwa akiziwakilisha nchi zao nchini, Roeland van de Geer aliondolewa kwa shinikizo la Serikali.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alikanusha Serikali kumshinikiza balozi huyo kuondoka, badala yake alisema ameitwa na mabosi wake huko Brussels, Ubeligiji kuzungumzia hali ya siasa.

Lakini katika tamko la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) lililoandikwa Desemba 12, jumuiya hiyo pamoja na mambo mengine, imelalamikia Balozi De Geer kuondolewa kwa shinikizo ikiwataja pia wanadiplomasia wengine iliyodai pia waliondolewa kwa shinikizo kuwa ni pamoja na waliokuwa viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wakiwamo Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Mbowe na Matiko wala Krismasi na mwaka mpya rumande

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko wamejikuta wakila Sikukuu ya Krismasi na pengine mwaka mpya rumande baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha kesi yao Desemba 21 hadi Januari 3, mwakani.

Mbowe na Matiko wako katika Gereza la Segerea baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23 kwa kukiuka masharti ikiwamo kutoka nje ya nchi bila kibali.

Yeye na viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi na kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa, hakuweza kufika mahakamani wakati kesi yao ilipotajwa na kusababisha dhamana yao kufutwa.

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ya jinai namba 112/2018 ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na manaibu katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Wengine ni wabunge wa chama hicho Halima Mdee (Kawe), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na John Heche (Tarime Vijijini).