VIDEO: ATCL: Diamond alichelewa kufika Uwanja wa Ndege

Muktasari:

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema mwanamuziki Diamond Platnumz hakuachwa na ndege ya shirika hilo bali alichelewa kufika uwanjani

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema mwanamuziki Diamond Platnumz aliyekuwa miongoni mwa abiria waliopaswa kusafiri na ndege ya shirika hilo jana Desemba 16, 2018  hakuachwa kama inavyoelezwa bali alichelewa.

Limesema Diamond na abiria wengine walichelewa na tiketi zao hazikuuzwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 17, 2018 mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa ATCL, Josephat Kagirwa amesema shirika limelazimika kutoa ufafanuzi kwa umma baada ya kuona malalamiko ya Diamond yakisambaa maeneo mengi kupitia mitandao ya kijamii.

“Tiketi ya Diamond ambayo ina jina la Isack Nasibu ilionyesha kuwa alikuwa anatoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kwa ndege yetu namba 103 jana jioni,” amesema.

“Muda wa kufika uwanja wa ndege umeelezwa kuwa ni masaa mawili kabla ya muda wa safari. Yeye alifika akiwa amechelewa hivyo alizuiliwa na mamlaka za viwanja vya ndege kwa mujibu wa taratibu.”

Amesema tiketi za shirika hilo zinaruhusu abiria kutumia tiketi yake ambayo hakuitumia siku husika na hata Diamond ameomba kutumia tiketi hiyo leo jioni.

“Tiketi ya mteja haiwezi kuuzwa. Ila asipoonekana uwanjani na akawepo mtu mwingine anahitaji huduma tutampa nafasi maana nafasi katika ndege thamani yake inaisha ndege inaporuka lakini tiketi baada ya hapo inabadilishwa,” amesema Kagirwa.