AU yatoa tamko uchaguzi DRC

Muktasari:

Rais Cyril Ramaphosa ameipongeza DRC kwa kuandaa uchaguzi na kutoa wito kwa mataifa ya kimataifa kujizuia na kuwaacha maofisa wa tume ya uchaguzi kumaliza kazi yao



Kinshasa,DRC. Umoja wa Afrika umetoa wito kwa migogoro yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutatuliwa kwa njia ya amani na majadiliano.

Taarifa kutoka ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat imesema ni muhimu tofauti zozote kuhusu matokeo yaliotangazwa, kwamba hayakuakisi matakwa ya wapigakura, zitatuliwe kwa amani,  sheria husika na kupitia majadiliano ya kisiasa kati ya vyama vinavyohusika.

Kanisa Katoliki nchini humo limesema matokeo ya awali hayawiani na takwimu ilizokusanya huku Ufaransa ikisema inaamini mgombea mwingne wa upinzani Martin Fayulu ndiye alieshinda kihalali.

Mahamat amesema amezingatia matokeo ya awali bila kujali matokeo ya mwisho ya uchaguzi, DRC inapaswa kutafuta muafaka wa kitaifa kwa msingi wa kuheshimu kanuni za demokrasia na haki za binadamu pamoja na kulinda na kuimarisha amani.

Umoja wa Ulaya(UN) umesema unafuatilia matokeo ya kushtukiza ya uchaguzi huo na pia kutilia matamshi ya waliochukua nafasi ya pili katika uchaguzi huo walioyafananisha matokeo hayo na mapinduzi.

Msemaji wa Halmashauri ya UN Maja Kocijancic amesema kwa sasa wanasubiri ufafanuzi kutoka kwa waangalizi wa kimataifa huku ikizitaka pande zote kujiepusha na vurugu.

Afrika Kusini imeiomba CENI kukamilisha utoaji wa matokeo kwa uaminifu na kuzingatia amani na uthabiti wa nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reynders amesema nchi yake inapanga kuliwasilisha suala la DRC katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Ubelgiji imekuwepo kwa miaka miwili sasa.