Adaiwa kusafirisha mirungi akijifanya mjamzito

Frola Mwita (aliyejishika kifuani) Mwanamke anayedaiwa kunaswa na kilo 8 za mirungi akijifanya mjamzito kitokea Tarime mkoani Mara kwenda jijini Mwanza. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Frola Mweita (40) mkazi wa Tarime mkoani Mara amekamatwa akituhumiwa kusafirisha kilo nane za mirungi, akiwa amezifunga tumboni na kuonekana kama mjamzito

Mwanza. Frola Mweita (40) mkazi wa Tarime mkoani Mara amekamatwa akituhumiwa kusafirisha kilo nane za mirungi, akiwa amezifunga tumboni na kuonekana kama mjamzito.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 10, 2018  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,  Jonathan Shanna amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafirisha  mirungi hiyo kutoka Tarime kwenda Mwanza, akiwa katika basi la kampuni ya mabasi ya Zakaria.

“Alikamatwa Nyakato jana na mirungi na alikuwa ameifunga  tumboni na kuonekana kama mjamzito,” amesema Shana

Mbali na mtuhumiwa huyo, watu watatu, wakiwemo wanafunzi wawili wamekamatwa wakiwa na kilo 12 za mirungi.

Amesema watu hao walikamatwa Desemba 9, 2018  baada ya polisi kupata taarifa kwamba kuna watu wanaojihusisha na biashara hiyo.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Fatiha Saba (15) mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari ya Thaqaafa, Karen Saba (13) mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Musabe na Saad Kapinga (49).