Ahadi za wateule wa Magufuli

Muktasari:

Mawaziri na Manaibu mawaziri wapya wameapishwa Jana Ikulu Jijini Dar es salaam huku wakitoa ahadi mbalimbali kwa Rais Magufuli.

Dar es Salaam. Mawaziri na manaibu waziri waliopaishwa jana siku mbili baada ya kuteuliwa, wameahidi kufanya kazi kufa au kupona ili kukidhi matarajio ya Rais John Magufuli.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema ataanza na mambo matatu, maagizo ya korosho waliyopewa na Rais yanayoanza utekelezaji bila kukaa chini.

Alisema jambo lingine ni ufuatiliaji wa upatikanaji wa pembejeo. “Katika baadhi ya mikoa mvua zimeanza kunyesha lakini kilio cha wakulima ni pembejeo, hili kwangu ni muhimu zaidi, ”alisema.

Pia, alisema atashirikiana na wizara nyingine ikiwamo ya biashara kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya bidhaa zao.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa alisema atashirikiana na waziri wake kuhakikisha viwanda vinatokea shambani kwa kuzalisha malighafi ya kutosha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alisema miongoni mwa maagizo waliyopewa na Rais ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii kutoka asilimia 17 ya sasa na kuweka miundombinu mizuri kwa watalii na usalama wao akiahidi pia kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu uvamizi wa misitu na maeneo ya hifadhi.

Mwita Waitara ameteuliwa kuwa naibu waziri wa Tamisemi alisema kama atatakiwa kufanya kazi usiku na mchana yupo tayari kufanya hivyo.

“Ninachoomba ni ushirikiano kwa nitakaowakuta na nitafanya kazi iliyotukuka kwa sababu masuala ya Tamisemi sina ugeni nayo, nimekuwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na mbunge, hivyo nafahamu baadhi ya mambo,” alisema.

Mary Mwanjelwa, aliyehamishiwa Utumishi kuwa naibu waziri, alisema atafuatilia upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wanaostahili.

“Wapo watumishi wwenye sifa na uwezo, lakini wamefanya kazi sehemu moja kwa muda mrefu, nitahakikisha wanapanda madaraja,” alisema Mwanjelwa.