Akatwa vidole na mume

Rose Mgendi(24) akiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara alikolazwa baada ya kukatwa vidole viwili vya mkono wa kushoto na mume wake kutokana na mzolo wa wivu wa mapenzi kati yao.Picha na Beldina Nyakeke

Musoma. Desemba 7, yaweza kuingia katika orodha zenye kumbukumbu mbaya kwa Rose Mgendi (24), mkazi wa Butiama.

Siku hiyo haikuwa nzuri, kwani alipoteza vidole viwili vilivyokatika wakati wa ugomvi baina yake na mumewe.

Mkazi huyo wa Kijiji cha Nyabange aliingia kwenye ugomvi na mumewe, anayeitwa Mariogo Mashele kutokana na kitendo chake cha kwenda ngomani bila ya ruhusa na kurudi usiku.

Kwa sasa, Rose amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara akiendelea na matibabu.

“Siku hiyo mume wangu alirudi nyumbani kutoka katika mizunguko yake majira ya saa 3:00 usiku na kunikuta anawasha moto kwa ajili ya chakula cha usiku,” alisema Rose alipozungumza na Mwananchi.

Anasema mumewe alimuita ndani, lakini akamuomba amsubiri amalize kuwasha moto na baada ya kumaliza aliingia kumsikiliza na ndipo mzozo ulipoanza.

“Aliniambia kuwa nina kiburi na simuheshimu,” alisema Rose akimnukuu mumewe.

Baadaye akaanza kumpiga akitumia panga huku akimfokea, lakini alifanikiwa kumponyoka na kukimbilia kwenye nyumba ya mama mkwe wake.

Mwanamume huyo alimfuata akiwa na panga lake na kuendelea kumpiga akitishia kumkata shingoni. Ili kujiokoa alilidaka panga eneo lenye makali na mumewe akalivuta na kusababisha vidole vyote vya mkono wa kushoto kujerujiwa huku viwili vikikatika.

Wakati mwanamke huyo akieleza kuwa alishambuliwa kwa sababu ya kuchelewa kuitikia wito, kamanda wa polisi wa mkoa, Juma Ndaki alisema pamoja na kuendelea kumsaka mumewe, Rose ndiye alikuwa chanzo cha ugomvi huo.

Alisema siku hiyo, Rose alichelewa na alirudi nyumbani usiku akitokea katika sherehe za kimila za tohara zinazoendelea wilayani humo.

“Kitendo hicho kilimkera mume wake na akamtuhumu kuwa na mahusiano na wanaume wengine,” alisema Kamanda Ndaki.

“Inadaiwa huyu mama alienda kwenye ngoma ya Litungu bila ridhaa ya mume wake, akachelewa kurudi hivyo mume akataka kumkata shingo lakini alikwepa.”

Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa, Dk Joachim Eyembe alisema walimpokea mwanamke huyo Ijumaa usiku akiwa amelewa na hajitambui.

Alisema licha ya kufika hospitalini hapo akiwa amelewa, alipata huduma zote ikiwemo ya upasuaji bila malipo baada ya kubainika kuwa hakuwa na fedha za kulipia matibabu.

Alisema tangu apatiwe matibabu, hali yake inaendelea vizuri.