Alichokisema Rais Magufuli mradi wa kuzalisha umeme

Muktasari:

Rais John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge kati ya Serikali ya Tanzania na Misri, kueleza jinsi mradi huo ulivyo rafiki katika utunzaji wa mazingira tofauti na baadhi ya watu wanavyodai kuwa unaharibu mazingira


Dar es Salam. Rais John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge kati ya Serikali ya Tanzania na Misri, akibainisha kuwa mradi huo utasaidia kutunza mazingira tofauti na baadhi ya wanamazingira wanavyokosoa.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 12, 2018 Ikulu Dar es Salaam katika utiaji saini huo ulishuhudiwa pia na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly, Magufuli amesema mradi  ulipigwa vita kwa kisingizio cha kulinda mazingira na kusisitiza kuwa unalenga kutunza hayo mazingira.

“Mradi huu umepigwa vita sana kwa hiyo sishangai kama mawazo haya ya Baba wa Taifa (Julius Nyerere) tangu mwaka 1970 leo ndiyo tunakuja kuweka saini zaidi ya miaka 40, nilijua matatizo waliyokuwa wanapambana nayo,” amesema.

“Nafahamu wapo wanaosema mradi huu utaharibu mazingira, hiyo si kweli hata kidogo. Ninavyojua mradi huu utasaidia kutunza mazingira.”

Ameongeza, “kwanza ni  kwa sababu umeme wa maji ni rafiki wa mazingira, pili eneo la kutekeleza mradi huu ni dogo ambalo ni asilimia 1.8 hadi 2 ya eneo zima la Selous ambalo ni kubwa kuliko baadhi ya nchi.”