Aliyejiuzulu ubunge CUF aomba kujiunga CCM

Aliyekuwa mbunge wa Temeke (CUF) Abdalah Mtolea

Muktasari:

  • Aliyekuwa mbunge wa Temeke (CUF) Abdalah Mtolea leo Alhamisi Novemba 15, 2018 ameomba kujiunga na CCM akiwa ofisi za makamo makuu ya chama hicho jijini Dodoma

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Temeke (CUF) Abdalah Mtolea ambaye leo Alhamisi Novemba 15, 2018 ametangaza kujizulu, ameomba kujiunga na CCM.

Mtolea ametangaza uamuzi wa kuomba kujiunga na chama hicho jioni ya leo Alhamisi  makao makuu ya CCM jijini Dodoma mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally.

Dk Bashiru amemwelekeza Mtolea kwenda katika tawi lililo karibu na makazi yake wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam ili afuate utaratibu wa kuomba uanachama wa CCM.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesisitiza leo Alhamisi Novemba 15, 2018 ndio siku ya mwisho kupokea viongozi wa upinzani wanaoomba kujiunga na chama hicho.

Akizungumzia uamuzi wake wa kujiuzulu na kuomba kujiunga na chama dola, Mtolea amesema amevutiwa na mageuzi makubwa ya kiuongozi na kazi nzuri inayofanywa na CCM na Serikali yake chini ya Rais John Magufuli.