Aliyesamehewa na JPM bado hajatema nyongo

Muktasari:

Mwaka 1974 Matonya alihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupa-tikana na hatia ya kuua ingawa adhabu yake ilib-adilishwa na kuwa kifungo cha maisha.

Chamwino. Kuna jambo bado linamkereketa Mganga Matonya, mzee wa miaka 86 aliyekuwa amefungwa lakini akaokolewa na msamaha wa Rais John Magufuli Desemba 11 mwaka jana.

Matonya alikuwa mmoja kati ya zaidi ya wafungwa 8,000 waliosamehewa na Rais mwishoni mwa mwaka jana. Alikuwa akitumikia kifungo cha maisha lakini akatumikia kwa miaka 43 kabla ya kupata msamaha huo.

Awali, pamoja na wenzake wawili, Matonya alihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua wakati akijaribu kuiba ng’ombe 12.

Tangu atoke Gereza la Mkono wa Simba mkoani Morogoro, Matonya amekuwa kijijini kwake wilayani Chamwino akijaribu kuzoea maisha mapya baada ya yale ya wizi kusababisha afungwe kuanzia mwaka 1974.

Lakini jambo moja ambalo lilikuwa likimuumiza na hadi sasa linaendelea kumsumbua moyoni mwake; “ni wapi atakutana na Rais Magufuli” ili ateme nyongo yake.

“Bado ninalo neno la kumwambia Rais Magufuli (John) kama nitakutana naye,” alisema Matonya baada ya Mwananchi kumfuata nyumbani kwake Kijiji cha Wiliko kilichoko takriban kilomita 81 kutoka Dodoma Mjini.

“Bado nina hamu ya kumuona Rais John Magufuli. Mungu akinichukua nitakwenda na maneno yangu moyoni.”

Kauli hiyo, ambayo alikuwa akiirudiarudia katika mazungumzo na Mwananchi inalingana na ile aliyoitoa mwaka jana mara baada ya kufika kijijini akitokea gerezani.

“Kama nitashindwa kumuona (Rais), nitabaki na neno hilo moyoni mwangu. Ila Watanzania wajue kuwa niliua kweli, naomba Mungu anisamehe na wao wanisamehe pia,” alisema Mganga wakati huo.

Hata hivyo, Mganga hakutaka kueleza neno hilo linahusu nini na kwanini anaamini kuwa Rais Magufuli ndiye mtu pekee anayefaa kuelezwa neno hilo.

“Siwezi kumwambia hata mwanangu, lakini kama nilivyokuambia mwaka jana kuwa nina mambo mawili, moja ni langu binafsi na la pili ni muhimu kwa Taifa,” alisema.

“Iko siku nitakutana na Rais na nitamwambia niliyonayo moyoni pamoja na kuwasaidia walioko magerezani.”

Mkewe anayeitwa Nyendo anatamani pia mumewe atimize ndoto yake ya kumuona Rais.

“Ni afadhali akutane na Rais Magufuli ili apungue mawazo. Amekuwa akinisumbua kila mara akisema ana ndoto za kumuona Rais,” alisema Nyendo, mama wa watoto sita na zaidi ya wajukuu 34.

Hata hivyo, anasema Rais alishafanya kazi yake ya kumsamehe kifungo hivyo kama ana jambo ni bora awaambie viongozi wa chini walimalize.

Matonya na wenzake wawili walishtakiwa mahakamani baada ya kutuhumiwa kuwa walimuua mtu mmoja aliyekuwa akimiliki ng’ombe wakati walipokwenda kuiba mifugo hiyo.

Matonya alifanikiwa kutoroka eneo la tukio, lakini polisi walimsaka na kufanikiwa kumtia mbaroni kabla ya kumpeleka mahakamani ambako alipata adhabu hiyo ya kifo ambayo baadaye iligeuzwa na kuwa kifungo cha maisha.

Tofauti na alivyokuwa mwaka mmoja uliopita alipotoka gerezani, Matonya anaonekana kuwa na afya njema na uso wake unapambwa na tabasamu wakati wa mazungumzo, ingawa kumbukumbu zake kichwani zinaonekana kuwa mbali.

“Kwa sura siwezi kukukumbuka, lakini nahisi kuna mahali nilikuona,” alisema Matonya baada ya kusalimiwa na mwandishi wa Mwananchi.

“Sijui ni gerezani ama wapi, hebu nikumbushe… Ah kumbe ni wewe tena ulifungua milango wakaja watu wengi hapa ikawa kama mjini.”

Tofauti na alipotoka gerezani, Matonya amevalia kwa unadhifu na anaongea na wanawe huku wakicheka.

Katika mazungumzo yetu kuhusu maisha yake tangu atoke gerezani, Matonya anasema bado ni mazuri na hana hofu kwani anaamini yaliyotokea yalikuwa ni mambo ya ujana na kwamba jamii ilishamsamehe na Mungu pia alimsamehe kutokana na kujutia makosa yake.

“Ninashirikiana vizuri na majirani na Serikali ya kijiji changu na natimiza ahadi ya kuwa raia mwema na mtoa ushauri kwa makundi mbalimbali kijijini ili wawe raia wema,” alisema.

Lakini anashangaa tangu atoke gerezani, hajawahi kuona mwanga wa umeme mahali popote kwa kuwa kijijini kwao umeme haujafika.

Pia makazi yake bado hayamfurahishi.

“Kinachonisumbua ni makazi tu,” alisema.

“Naishi katika nyumba iliyochoka sana, uwezo wa kuikarabati sina na nguvu zimeisha. Sasa hili tembe likiporomoka itakuwa hatari kwangu, mke wangu na wajukuu wanaolala hapa, labda Mungu aendelee kunilinda mimi na mke wangu.”

Lakini akikumbuka maisha ya gerezani, Matonya anaona ni afadhali aendelee kuishi maisha ya sasa uraiani kuliko alipokuwa kifungoni.

“Kule hakufai, hakuna uhuru, hakuna masikilizano, yaani kuna utofauti mkubwa na huku uraiani,” alisema.

“Askari magereza wanafanya kazi ngumu sana maana kwenye mchanganyiko wa watu kuna shida kwa ujumla.

“Siwezi kukumbuka kitu mle ndani zaidi ya kuwaombea ndugu na vijana wangu niliowaacha. Ninaamini itachukua muda mrefu wengi kurudi uraiani. Nikilala nawaota sana na ninakumbuka mazungumzo yetu ya kufarijiana ambayo nilikuwa naongoza mimi.”

Mkewe anayeitwa Nyendo sasa amepata faraja baada ya Matonya kurejea uraiani.

“Maisha yamebadilika kiasi ukilinganisha na kipindi ambacho (Matonya) alikuwa gerezani. Watoto walikuwa wakinisaidia mambo mengi, lakini sikupata mtu wa kufarijiana naye kama ilivyo kwa sasa,” alisema Nyendo.

Diwani wa Kata ya Mlowa Bwawani, Andrew Msewa anasema Matonya ni miongoni mwa wazee wenye busara na hekima ambao wanafaa kuombwa ushauri katika kipindi ambacho mambo yanakuwa magumu.

Msewa anasema Matonya amekuwa mtu wa simulizi na mtu anayetoa mchango wa mawazo, lakini kila mara akisisitiza haja yake ya kumuona Rais Magufuli.

“Nachoweza kumsaidia ni kumfikisha kwa mkuu wa wilaya ili kutafuta namna ya kumuona Rais,” alisema.