Atupwa jela miaka 30 kwa kumuoa mwanafunzi

Muktasari:

  • Mahakama iliyakataa maombi ya watuhumiwa ikisema makosa ya kubaka na kuwapa mimba wanafunzi yamekuwa yakiongezeka wilayani humo.

Misungwi. Mahakama wilayani Misungwi mkoani Mwanza, imemhukumu Nyanda Zephania (27), mkazi wa Kijiji cha Inonelwa kwenda jela miaka 30 na kulipa faini ya Sh50,000 kwa makosa matatu ya kumtorosha, kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Erick Marley aliwatia hatiani watuhumiwa wengine watatu kwa makosa hayo.

Wengine ni George Kazula (56), Melesiana Nyanda (50) na Lucas Zabalana (45) ambao mahakama iliwaona wana kosa moja la kula njama ya kumtorosha mwanafunzi huyo kwa wazazi wake na kumwachisha masomo ya sekondari aliyokuwa akisoma katika Sekondari ya Misasi.

Walihukumiwa kifungo cha mwaka moja jela au faini ya Sh50,000 kila mmoja.

Hakimu Marley alisema kwa mujibu wa ushahidi ambao haukuacha shaka, washtakiwa kwa pamoja walikubaliana kumshawishi na kumwachisha masomo ya kidato cha kwanza mwanafunzi huyo ili akaolewe na Zephania. Awali, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Ramso Salehe alidai mahakamani hapo kuwa mwanafunzi huyo alitoroshwa Machi 2017 na kupatikana Mei mwaka huu akiwa na ujauzito.

Mahakama iliwapa nafasi ya kujitetea washitakiwa ili wapunguziwe adhabu. Zephania aliiomba mahakama imsamehe na watuhumiwa wenzake watatu.

Mahakama iliyakataa maombi ya watuhumiwa ikisema makosa ya kubaka na kuwapa mimba wanafunzi yamekuwa yakiongezeka wilayani humo.

Hivyo iliwahukumu pia watuhumiwa wa pili, tatu na nne kulipa kila mmoja faini ya Sh50,000 au kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kumtorosha mwanafunzi huyo kwa wazazi wake na kumpeleka katika machimbo ya Lwamgasha mkoani Geita alikokukutana na Zephania na kuoana naye.

Washtakiwa hao walilipa faini na kuachiwa huru na kumwacha Zephania akienda gerezani kutumikia kifungo chake.