Awamu ya kwanza SGR kukamilika mwakani

Muktasari:

  • Ujenzi wa Reli ya Kisasa utaiingiza Tanzania katika moja ya nchi chache Afrika ambazo zimewekeza vya kutosha katika sekta ya miundombinu.

Dar es Salaam. Sehemu ya kwanza ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro inatarajiwa kukamilika Novemba 2, mwakani wakati ile itokayo Morogoro hadi Makutupora Dodoma ikimalizika Februari 2021.

Ujenzi wa awamu zote mbili unatarajia kutumia Sh7.1 trilioni ambazo zimetokana na kodi ya Watanzania.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),Masanja Kadogosa amesema jijini leo kuwa ujenzi huo unafanywa kwa vipande vipande ili kuharakisha mradi huo ukamilike kwa wakati.

"Kila kipande kinasimamiwa na meneja wake na tunafanya hivi ili twende na wakati kwani kila kipande kitajengwa bila kuathiri kipande kingine," amesema.

Amesema hadi sasa ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar- Morogoro umekamilika kwa zaidi ya asilimia 34.

Amesema jumla ya madaraja 26 yanatarajiwa kujengwa ili kukamilisha awamu hiyo ya kwanza hadi Morogoro.

" Zaidi ya yote ujenzi huu umetoa ajira 6,500 kwa watu mbalimbali kama madereva, wahandisi na mafundi," alisema.