Barabara inayojenga SGR ni habari nyingine kabisa

Muktasari:

  • Kukamilika kwa Reli ya Standard Gauge (SGR), sio tu kutarahisisha usafiri na usafirishaji kwa njia ya reli bali pia kutakuwa kumet-engeneza barabara mpya ambayo kwa sasa inatumika kwa ajili ya shughuli za ujenzi huo.

Dar es Salaam. Nilipoanza safari ya kutembelea ujenzi wa Reli ya Standard Gauge (SGR) unaoendelea kati ya Dar es Salaam na Dodoma, sikujua kama ningeweza kupita kwa gari ili kuona kazi inavyoendelea.

Kuanzia ulipoanzia ujenzi wa reli hiyo Gerezani jijini Dar es Salaam nikiwa ndani ya gari, nilijua tutapita maeneo machache kujionea ujenzi unavyoendelea bila kujua kuwa kuna barabara imetengenezwa pembezoni mwa ujenzi wa reli hiyo kuanzia Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma.

Safari ilipoanza Gerezani hadi stesheni ya Pugu umbali wa kilomita 20, tulipita katika barabara iliyochongwa pembezoni mwa reli ya zamani inakojengwa SGR huku tukipishana na malori, magari madogo na mabasi ambayo yote yanafanya kazi kwenye mradi huo.

Kuanzia kilomita 20 Pugu stesheni hadi kilomita 53 Soga stesheni, Kibaha mkoani Pwani kutokea Dar es Salaam, barabara hiyo imechongwa kwenye vilima na kupita katika mabonde.

Katika baadhi ya maeneo vilima vimechongwa ili kuwezesha reli hiyo kupita, majani yameoteshwa kwenye kingo za vilima hivyo ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Baada ya kufika Soga nilijua tunaachana na reli kisha kwenda barabara kuu ya Mororogo ili kuendelea na safari, lakini meneja mradi wa ujenzi wa reli hiyo awamu ya kwanza Dar es Salaam- Morogoro, Masanja Machibya anatuambia tunaendelea kupita kwenye barabara iliyoko pembezoni mwa reli hadi Morogoro.

Safari inaendelea kutoka kilomita 53, stesheni ya Soga hadi kilomita 90 stesheni ndogo ya Kwala Kibaha ambako tunakuta ujenzi wa karakana kubwa ya ukarabati wa treni na ujenzi wa bandari kavu.

Barabara hiyo tuliyokuwa tukipita, imechongwa vizuri na magari yanaweza kutembea eneo tambarare mwendokasi wa mpaka kilomita 120 kwa saa.

Kutoka Kwala safari inaendelea hadi Ngerengere mkoani Morogoro, ambako kuna kambi kubwa ya wafanyakazi wa ujenzi wa reli hiyo.

Baada ya kufika Ngerengere kwa kuwa ilikuwa jioni na kazi zilishafungwa tunaamua kwenda Morogoro kwa kurudi kwenye barabara kuu ya Morogoro.

Siku iliyofuatia tunaendelea na safari yetu kutoka Morogoro katika eneo ambalo ujenzi wa awamu ya pili unakoanzia hadi Dodoma.

Tunaanzia sehemu ambayo ujenzi wa awamu ya kwanza utaishia, kilomita 201.819 chini ya usimamizi wa meneja mradi Machibya.

Katia sehemu ya pili ya safari yetu Morogoro-Dodoma sasa tupo chini ya meneja wa mradi huo awamu ya pili, Faustine Kataraiya ambaye anasimamia kilomita 482 za reli hiyo.

Safari inaanza kupitia barabara ambayo eneo kubwa ni tambarare tofauti na ilivyo kati ya Pugu hadi Soga na inatufikisha katika vilima vya Kilosa ambako kunafanyika utoboaji wa kilima eneo lenye umbali wa kilomita 2.5 ili treni hiyo iweze kupita.

Kwa wale ambao hawaelewi kwa nini treni ni lazima ipite katikati ya kilima, hatua hiyo inalenga kuepusha changamoto ya mafuriko inayoikumba reli ya kati hivi sasa. Eneo hilo la Kilosa ndilo ambalo mafuriko hutokea kutokana na mto Kidete kumwaga maji mengi wakati wa mvua na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya reli ya kati.

Hadi kufika eneo ambalo kilima hicho kitatobolewa, kuna barabara imechongwa katika vilima vya kilosa ikiwa na uwezo wa kupishana magari mawili. Kwa sasa eneo hilo ndipo barabara imeishia ikisubiri kutobolewa kwa baadhi ya vilima ili iendelee na safari.

Hapa barabara inakwama hivyo inabidi twende Dumila na kwenda hadi Mpwapwa kwenye stesheni ya Gulwe ambako barabara hiyo inaendelea huku maandalizi ya ujenzi yakifanyika hadi Ihumwa mkoani Dodoma kunakojengwa kambi kubwa ya wafanyakazi wa ujenzi wa reli hiyo. Kutoka Ihumwa ni kama tayari umeshaingia Dodoma mjini kwani ni mwendo wa nusu saa tu.