Basata yasema Harmonize anavuna alichopanda Nairobi

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema mwanamuziki huyo aliondoka nchini kimya kimya kinyume na utaratibu.


Dar es Salaam.Baraza la Sanaa la Taifa(Basata), limesema halikutoa kibali cha kwenda kufanya shoo nchini Kenya kwa mwanamuziki  Harmonize na kwamba linashindwa kuingia kati kumsaidia katika masaibu yaliyompata.

Kauli ya Baraza hilo inakuja ikiwa ni siku chache tangu Harmonize apate matatizo ya kutapeliwa na mapromota waliomuita kufanya jambo lililomfanya ashindwe kufanya shoo katika Mji wa Eldoreti nchini humo.

 “Hii  ni dalili ya kunivunjia heshima na uaminifu kwa mashabiki zangu, imeniumiza kuona watu waliojitoa kulipa viingilio vyao kwa ajili yangu wanadhulumiwa mwisho kabisa. Niseme samahani Eldoret, siku nyingine nitahakikisha tumelipwa hela yote kabla ya kuja, naomba  mniamini nimeumia sana na ninawapenda,” aliandika Harmonize katika mtandao wa Instagram.

MCL Digital ilimtafuta Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza ambao ndio walezi wa wasanii kama wana taarifa kuhusu sakata hilo.

Mngereza alisema ndio kwanza anazisikia taarifa hizo na isitoshe Harmonize hajapita kwao kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kwenda kufanya shoo kama ambavyo sheria inataka.

“Kiutaratibu kabla ya msanii kwenda kufanya shoo nje ya nchi anatakiwa apate kibali kutoka Baraza, sheria ambayo ipo tangu mwaka 1974, lakini hatujui ni kwa nini wasanii wengi wanalikwepa hilo wakati ni jambo ambalo halichukui hata saa moja, halafu wakishapata matatizo huko ndio wanarudi kwetu, naomba wabadilike katika hili ili wie rahisi kuwasidia wanapokumbana na misukosuko ya hapa na pale,”alisema Mngereza.

Anabainisha kuwa baadhi ya wasanii ili kukwepa kupita katika utaratibu huo, wengi wakifika uwanja wa ndege wanasema kuwa wanasafiri kwa shughuli zao binafsi ili wasiulizwe kibali cha Basata kipo wapi, jambo ambalo ni hatari kwani wakipata matatizo si rahisi serikali  kuwasaidia kwa kuwa hawakuwa  na taarifa.

Mmoja wa wakurugenzi katika lebo ya wasafi ambapo msanii huyo anafanyia kazi, Hamis Taletale 'Babu Tale' alijibu kwa kifupi kuwa kilichompata msanii wao Harmonize nchini Kenya hawakitambui na wao wanachosubiria ni fedha.

Babu Tale, alisema kilichotokea kwa Harmonize na wao wamesikia kama watu wengine kwenye mitandao na kuongeza kuwa msanii huyo ana meneja wake hivyo na wao wanasubiri waletewe taarifa nini hasa kiliwapata na isitoshe wanachohitaji ni fedha.