Bashuru Ally awashukia wanaomchafua mitandaoni

Muktasari:

  • Baada ya kusambaa kwa andiko katika mitandao ya kijamii likionyesha kutolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, amezungumza na Mwananchi na kueleza kuwa andiko hilo si lake, kwamba limewekwa na watu waliozoea kuendesha nchi kiholela.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally amewashukia baadhi ya watu walioweka andiko mtandaoni likionyesha kuwa amemjibu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Desemba 4, 2018 Dk Bashiru amesema andiko hilo si lake na hayupo katika mfumo wowote unaomuwezesha kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii zaidi ya kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno.

Sehemu ya andiko hilo linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii linasema, “Zipo taarifa kwamba yupo kiongozi mmoja aliyewahi kuwa mwandamizi wa Taifa hili eti kanikosoa kuhusu utaratibu niliotumia kumwita ndugu Membe, mimi niombe hawa wastaafu watulie ili tukiweke chama sawa.”

“Na nirudie tu kusema ndugu Membe kama atakuwa hajafika ofisini kabla ya tarehe 17 na 18, 2018 nitakiomba kikao cha kamati kuu ya NEC kimwazimie.”

Dk Bashiru amesema waliofanya hivyo ni wale waliozoea kuendesha nchi kiholela na bado watazua mengi.

“Vyombo vya habari jitahidini kuelimisha wananchi kama kweli mna mapenzi na nchi hii,  huko kwenye mitandao hakuna weledi wala maadili ni upotoshaji umejaa huko, ”amesema.

Amesema kuendekeza mitandao nchi imekuwa si salama tena, mtu anaweza kuamua kusimamisha shughuli kwa maneno ya uchonganishi.

 “Watu wanaonijua wanafahamu jinsi ninavyotumia simu, sipo huko na  sina Instagram, Twitter, WhatsApp, Facebook wala mfumo wa barua pepe kwenye simu yangu, ni wazushi hao puuzeni hizo habari, ”amesisitiza.