Bavicha kusherehekea gerezani

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu siku ya Uhuru wa Tanzania Bara. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi amesema kufuatia kuahirishwa kwa sherehe za Uhuru, wamepanga kutembelea magereza mbalimbali nchini ili kuzungumza na wafungwa na mahabusu.

Sosopi amesema wameamua kufanya hivyo baada ya Serikali kutangaza kuahirishwa kwa sherehe za miaka 57 ya Uhuru, ambapo fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shamrashamra hizo zitatumika kujengea Hospitali ya Uhuru jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho jana, Sosopi alihoji kufutwa kwa sherehe hizo huku akisema Uhuru una maana zaidi hususan kwa vijana.

Alisema katika ziara yao magerezani kesho watapeleka ujumbe wa hali ya mambo ilivyo nchini kwa sasa.

Sosopi alielezea kushangazwa kwake na sherehe hizo kufutwa, lakini shughuli za kukimbiza Mwenge ambazo zinagharimu fedha nyingi zimefanyika.

“Tunawaomba Desemba 9 iwe siku muhimu sana kuwatembelea mahabusu na wafungwa,” alisema. Katika hatua nyingine, alilaani nguvu inayotumiwa na Jeshi la Polisi wakati wa usikilizwaji wa kesi zinazowakabili viongozi wa chama hicho.

Alimtaka msajili wa mahakama pamoja na Jaji Mkuu kutoa tamko juu ya kile alichoeleza kuwa ni uvunjwaji wa haki za msingi za raia katika kufuatilia mashauri mbalimbali kwenye mahakama nchini.

Sosopi alisema wanachukizwa na jeshi hilo kutumia nguvu kubwa kuwazuia watu wanaofika mahakamani kufuatilia kesi za viongozi wao.

Alisema tangu kesi hizo zilipoanza kusikilizwa Machi, baadhi ya wafuasi wao wanaojitokeza kufuatilia mahakamani wanakamatwa na kuhojiwa na jeshi hilo, jambo alilodai kuwa linaingilia uhuru wa mahakama.