Benki ya Dunia yaimwagia mabilioni Tanzania

Rais John Magufuli akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kwa Kanda ya Afrika, Hafez Ghanem Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa.

Muktasari:

  • Leo Ijumaa, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk  Hafez Ghanem.
  • Katika mazungumzo hayo, Benki ya Dunia imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani Milioni 300 sawa na Sh680.5 bilioni

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani 300 milioni sawa na Sh680.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.

Mradi huo unakusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia. 

Taarifa iliyotumwa leo Ijumaa Novemba 16, 2018 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais John Magufuli amekutana Ikulu jijini Dar es Salaam na  Makamu wa Rais wa WB Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem.

Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Amesema miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani 5.2 bilioni sawa na zaidi ya Sh13 trilioni inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri baina yake  na Tanzania.

Dk Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi.

Aidha amempongeza Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mzuri baina yake na Benki ya Dunia huku akiahidi Serikali itaendeleza na kukuza uhusiano huo.

Amesema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.

Namshukuru Dk Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali,” amesema.

Rais Magufuli amesema benki hiyo pia imetoa fedha zinazofadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.

“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 24, ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu ya kwanza na ya pili na miradi mingine mbalimbali.