BoT yazifungia benki tano kuuza, kununua dola

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa ya BoT, benki zilizofungiwa kufanya biashara ya ubadilishaji fedha kuanzia Novemba 23 ni Barclay, Exim, UBA, ABC na Azania.


Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezifungia kwa mwezi mmoja benki za kibiashara tano kutojihusisha na ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.

Hatua hiyo ya BoT inatazamwa kama mwendelezo wa chombo hicho kikuu cha usimamizi wa fedha kudhibiti biashara ya utakatishaji na ubadilishaji wa fedha kiholela.

Takriban wiki mbili zilizopita BoT iliyafungia maduka kadhaa jijini Arusha kwa madai kuwa yanaendesha shughuli zake kinyume na sheria zinazosimamia biashara hiyo, baada ya hapo ilitangaza kuwa huduma za ubadilishaji fedha zitapatikana katika hoteli za kitalii, benki na ofisi zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya BoT, benki zilizofungiwa kufanya biashara ya ubadilishaji fedha kuanzia Novemba 23 ni Barclay, Exim, UBA, ABC na Azania.

“Hatua hii imetokana na kuvunjwa kwa taratibu na kanuni, waliofungiwa walikuwa aidha wanafanya biashara kinyume na viwango vinavyowekwa au walikuwa hawawasilishi taarifa za miamala waliyokuwa wanafanya,” alisema Alexander Mwinamila ambaye ni mkurugenzi wa masoko ya fedha wa BOT.

Aliongeza kuwa hatua iliyochukuliwa inalenga kusimamia kanuni na taratibu za soko la ubadilishaji fedha za kigeni kwa mujibu wa sheria za nchi hii.

Mkuu wa masoko na mawasiliano wa benki ya Exim, Stanley Kafu alisema walipewa taarifa wiki iliyopita kuwa wao ni kati ya benki zilizozuiliwa kushiriki katika soko la ubadilishaji fedha za kigeni.

“Tuliarifiwa kuwa hatua imechukuliwa dhidi yetu kwa kuwa hatukuwasilisha Benki Kuu taarifa za miamala yetu ambayo tuliifanya kupitia soko la ubadilishaji wa fedha,” alisema Kafu wakati akiongea na Gazeti la Financial Times.