Bomba la mafuta hatihati

Muktasari:

  • Bajeti yake ni Dola 3.5 bilioni za Marekani unahusisha bomba lenye kipenyo cha inchi 24 lin-alotarajiwa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku, ulitarajiwa kujengwa na kukamilika 2020. lakini hoja za wawekezaji zina-onyesha dalili za kuuche-lewesha

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa imeanza kulipa fidia kwa wananchi walio katika maeneo litakakopita bomba la mafuta kutoka Tanga mpaka Hoima nchini Uganda, uhakika wa kukamilika mwaka 2020 upo shakani.

Hilo limebainishwa na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni alipokutana na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kujadili mustakabali wa mradi huo.

“Mpango wa mradi kukamilika mwaka 2020 una hatihati kwa sababu inahitaji miaka mitatu kukamilisha ujenzi wa miundombinu yake muhimu, mpaka sasa uamuzi wa kuwekeza haujafanyika,” alisema Irene.

Alifafanua kuwa ilitarajiwa uamuzi wa uwekezaji kufanyika mwaka jana ili ujenzi wa bomba hilo ukamilike mwaka 2020, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.

Irine alisema kinachosumbua ni makubaliano ya usimamizi na mgawanyo wa mapato baina ya wadau wakuu ambao ni Serikali za Uganda, Tanzania na kampuni zinazoshirikiana kutoa mtaji ambazo ni Total Oil ya Ufaransa, China National Offshore Oil Corporation na Tullow Oil ya Uingereza.

“Tunahitaji kuzungumza na kukubaliana ili kampuni hizi zitoe fedha. Serikali ya Uganda tumewasiliana na kampuni husika na kubainisha matarajio yetu. Kilichobaki ni kuyahuisha na ya Tanzania ili kila mmoja wetu awe na mkataba baina ya mwekezaji na nchi husika (HGA),” alisema.

Wakati Irene akiwa na wasiwasi huo, Dk Kalemani alisema Tanzania imeshakamilisha tathmini ya mazingira, jiolojia, fiziolojia na uthamini wa mali za wananchi waliopo eneo linakopita bomba hilo.

“Tulishaanza kulipa fidia kwa wananchi wa Tanga tangu mwaka jana na uchimbaji wa mtaro litakamopita bomba hilo umeanza kuanzia Tanga hadi Kondoa jijini Dodoma kupitia mkoani Manyara,” alisema Dk Kalemani.