Bosi NHC atangaza mabadiliko makubwa kiutendaji

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Nyumba la Taifa(NHC),Maulidi Banyana akizungumza na wafanyakazi wa Shirika hilo Leo,Oktoba 17,2018,Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk Maulid Banyani aliteuliwa Oktoba 30 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuliongoza shirika hilo.

Moshi. Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk Maulid Banyani amesema atafanya mabadiliko makubwa ya utendaji kazi kwa watumishi wote wa shirika hilo nchini ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Dk Banyani aliyeteuliwa Oktoba 30 kuliongoza shirika hilo, aliyasema hayo leo wakati akizungumza na wafanyakazi wa NHC mjini Moshi mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema wafanyakazi wa shirika hilo watarajie kuona mabadiliko hayo makubwa kwani katika ulimwengu wa sasa mabadiliko ni lazima yatokee kuendana na kasi ya Rais John Magufuli.

“Sasa hivi tutaanza kupima utendaji kazi wa kila mtu, jukumu lenu sasa hivi ni kuwa tayari kupokea mabadiliko hayo. Tutaanza kuhesabu utendaji kazi wa siku, lengo ni kujua kila siku ofisi zenu zinafanya nini,” alisema Dk Banyani na kuongeza:

“Nalipongeza shirika hili hapa mkoani Kilimanjaro kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuvuka asilima 100 ya ukusanyaji kodi, lakini niwaambie shirika hili litafanya mabadiliko makubwa, mkishuka chini ya asilimia 98 ya utendaji kazi nitashughulika na nyie.”

Alisema atafanya hivyo kwa sababu asilimia hiyo haitoshi inahitaji iwe zaidi ya hapo hilo kwani ndilo lengo la kila mwezi.

Alisema shirika hilo litaongeza miradi mbalimbali ambayo ina unafuu kwa wananchi wa ngazi zote ili liwe kimbilio kwa watu wote wanaohitaji huduma za makazi na biashara.

“Tunataka tuwe kimbilio la wananchi wote wa maisha ya chini, kati na juu, tutahakikisha bidhaa yetu ziwe na ubora wa kutosha wa hali ya juu ili itusaidie kutangaza biashara zetu za nyumba,” alisema.

Kwa upande wake, meneja wa shirika hilo mkoa wa Kilimanjaro, Juma Kiaramba alisema muda mfupi ujao shirika hilo litasaini mkataba mpya wa kujenga nyumba 25 za gharama nafuu ambazo zitagharimu Sh1.4 bilioni katika eneo la  shule ya sekondari Mawenzi ambapo majengo hayo yatachukua miezi 18 kumalizika kuanzia sasa.

“Mkoa wa Kilimanjaro ulichelewa kupata miradi kama hii kwa miaka nane iliyopita hivyo tunakuomba mkurugenzi utupe upendeleo kidogo wakutupa miradi mingine miwili katikati  ya miji huu," alisema Kiaramba.