Bunge Umoja wa Ulaya latoa maazimio 15 nchini

Dar es Salaam. Wakati Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) likipitisha azimio lenye vipengele 15 vinavyohusu Tanzania kwa kugusia masuala ya utawala wa sheria, haki za binadamu na kamatakamata ya wapinzani, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga amesema anasubiri maelekezo ya Rais kuzungumzia suala hilo.

Azimio hilo namba 2018/2969 ni mwendelezo wa hoja zilizowahi kuibuliwa na jumuiya hiyo ya kimataifa kuhusu Tanzania.

Hoja hizo zinahusu mambo kama haki za binadamu, masuala ya afya, elimu, haki za kupata habari, kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, mikutano ya kisiasa, sheria kandamizi na matamko.

Lakini Waziri Mahiga jana aliiambia Mwananchi kuwa hawezi kutolea majibu yoyote azimio hilo.

“Siwezi kuzungumzia lolote kuhusu hili. Bado nasubiri maelekezo kutoka kwa Rais. Eh nasubiri maelekezo ya Rais,” alisema kwa kifupi.

Bunge hilo la EU lilipitisha azimio hilo lililoandikwa Desemba 12, baada ya majadiliano yaliyofanyika mjini Brussels, Ubelgiji ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha kimataifa kutoa azimio dhidi ya Tanzania.

Huku likiwa limenukuu vifungu kadhaa vya kimataifa na kugusia uhusiano wake na Tanzania, azimio hilo ambalo limesambazwa sehemu mbalimbali linataka Tanzania irekebishe baadhi ya sheria.

Bunge hilo limebainisha matukio kama kupigwa marufuku mikutano ya kisiasa, kuandamwa kwa waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu, kufungia vyombo vya habari, kuzuia Bunge Live kuwa ni kati ya mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Azimio hilo limehoji kampeni iliyotangazwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuwasaka watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Azimio limetaka serikali imzuie Makonda kuendelea na kampeni hiyo.

Hata hivyo, hivi karibuni Serikali ilishabainisha kuwa kampeni hiyo haikuwa na ridhaa yake na alichokuwa akikifanya Makonda ni maoni yake binafsi.

Bunge hilo limetoa wito likitaka kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa, kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria, kama inayohusu makosa ya mtandao, sheria ya vyombo vya habari, Sheria ya Elektroni na Mawasiliano ya Posta(Epoca) na kuachiwa uwanja wa watetezi wa haki za binadamu kufanya shughuli zao.

Pia, limetaka tume huru itakayochunguza matukio yenye utata kama kutekwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari na matukio ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

“Tungependa kuona wale watakaobaini kuwa nyuma ya matukio hayo, hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao,” linasema azimio hilo.

Hii ni mara ya pili kwa EU kuelezea jinsi isivyoridhishwa na mwenendo wa Tanzania baada ya awali kumuita mwakilishi wake Brussels kwa ajili ya majadiliano.

Akizungumza baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu sakata hilo, Profesa Kitojo Wetengere wa Chuo cha Diplomasia (CFR) alisema Serikali isipuuzie azimio hilo.

“Kuna umuhimu wa kukaa meza moja ya majadiliano na EU ili serikali iwaelimishe kwa nini inafanya inachokifanya sasa,” alisema.