Butiku awasha moto wa Katiba mpya

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Bujiku akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na kongamano la kujadili mustakabali wa Taifa letu ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 10  tangu kifo cha Baba wa Taifa, litakalo fanyika Novemba 30-desemba 2. kushoto ni Kaimu Afisa utawala wa Taasisi hiyo. Picha na Peres Mwangoka

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ameungana na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba kuzungumzia suala la Katiba mpya akisema mjadala wa kuipata haujafa kwa sababu wenye Katiba ambao ni wananchi bado wanaishi.

Butiku, ambaye ni mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere kauli yake haijapishana na ya Jaji Warioba ambaye hivi karibuni alisema upo umuhimu wa Katiba mpya kwa kuwa ni maoni ya wananchi.

Novemba 2, Jaji Warioba aliliambia Mwananchi katika mahojiano maalumu kuwa kutokana na umuhimu huo kinachotakiwa kukubaliana ni lini na utaratibu gani utatumika kukamilisha mchakato wa Katiba hiyo.

Alisema maoni ya wananchi kwa kiwango kikubwa yapo kwenye Rasimu ya Katiba na mengineyo yaliingizwa kwenye Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, hivyo kinachotakiwa ni kukubaliana na utaratibu gani utumike ili kufikia mahitaji hayo.

Akizungumza jana wakati wa kumbukizi ya miaka mitano ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC), Dk Sengondo Mvungi, Butiku alisema Katiba ndiyo yenye misingi ya kuendesha nchi.

“Ninashauri tuendelee kuzungumza, kumuomba Mungu na kushauriana ili tupate Katiba mpya kwa sababu ndani ya Katiba ndiyo kuna misingi ya kuendesha nchi,” alisema Butiku.

Alisisitiza kwamba Katiba bora isipokuwepo, hulka za watu haziwezi kusimamiwa vizuri.

Alisema Watanzania wanahitaji Katiba ya kuwaonyesha namna ya kuendesha mambo yao hivyo ni vyema ikapatikana.

Novemba Mosi akiwa kwenye kongamano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais John Magufuli alipigilia msumari kwa kuweka wazi msimamo wake kuwa hayuko tayari kutoa fedha kwa ajili ya mchakato wa kupata Katiba mpya kwa sasa.

Alisema anafahamu kiu ya Watanzania ni kupatikana kwa Katiba, lakini mlolongo uliopo katika kuifikia hatua hiyo ndiyo unaomfanya aache mawazo hayo na kujikita zaidi kwenye shughuli za kuleta maendeleo.

“Nafahamu hamu ya Watanzania kuwa na Katiba mpya ila sasa tunafanyaje twende na Katiba pendekezwa au Rasimu ya Warioba, hapo ndipo ninapoona tuache kupoteza muda kutafuta majibu, tuchape kazi, tusitumie hela kuwalipa watu wakae vikao ni bora tukajenge reli. Kwa sasa sitegemei kutenga hela kwa ajili ya kuwapeleka watu kujadili Katiba na kama kuna mtu anataka kutupa hela kwa ajili hiyo azilete tutajengea reli,” alisema Rais.

Lakini jana Butiku alishauri kuanza kwa mjadala wa namna ya kupata fedha za kukamilisha mchakato wa Katiba mpya baada ya Rais kusema hakuna fedha za kuwalipa watu kujadili Katiba.

“Rais Magufuli alipokuwa Chuo Kikuu alisema anajua Watanzania wanahitaji Katiba mpya lakini hakuna fedha za kukamilisha mchakato huo kwa sababu haikuwa ajenda yake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Butiku.

“Tukizungumzia kuchangia kodi maalumu kwa ajili ya Katiba kuna tatizo?” alihoji Butiku huku akisisitiza kwamba Katiba bora ndiyo inabeba misingi ya uendeshaji wa nchi na wananchi wa Tanzania wanahitaji misingi hiyo iwekwe kwenye Katiba yao.

Akizungumzia kumbukizi ya Dk Mvungi, Butiku alimtaja kuwa mmoja wa watu waliokuwa na shauku kubwa ya kupata Katiba mpya na alifanya kazi kubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhakikisha inapatikana.

“Dk Mvungi hatunaye tena na hatujapata Katiba mpya. Hakufaulu lakini hajashindwa,” alisema Butiku na kuwataka Watanzania kuishi fikra zake kwa vitendo.

Naye mtoto wa Dk Mvungi, Dk Natujwa Mvungi alisema baba yake alikuwa mtu anayependa kusema na kutenda na shauku yake kubwa ilikuwa ni kuona Katiba mpya inayobeba masilahi ya wananchi inapatikana.

Dk Mvungi alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Novemba 12, 2013 baada ya kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake na kukatwa mapanga.