CCM yatoa msimamo vita ya Bashiru Ally na Membe

Muktasari:

Wakati vita ya maneno kati ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ikizidi kushika kasi, chama hicho tawala kimetoa ufafanuzi

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa msimamo wake dhidi ya vita ya maneno inayoendelea kati ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Taarifa iliyotolewa leo jioni Jumatatu Desemba 3, 2018 na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole inaeleza kuwa kauli ya Bashiru kumtaka Membe ambaye ni mwanachama wa chama hicho kufika ofisini kwake ni ya kawaida ndani ya CCM.

“CCM inapenda kuwafahamisha kuwa imefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wito alioutoa  Bashiru kwa Membe,” inaeleza taarifa hiyo.

“Ni kama sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama.”

Chama hicho kimetoa rai kwa Watanzania kuwa wito huo ulikuwa ni wa kawaida  hivyo uzushi, uchonganishi, fitina na uvumi mwingine wowote unaoendelea katika mitandao ya kijamii ina hila mbaya kwa CCM.

Katika taarifa hiyo Polepole amesema CCM inawataka Watanzania kuendelea kuwa na umoja, mshikamano na upendo katika kipindi hiki ambacho Rais John Magufuli  anaendelea kuongoza nchi katika mageuzi ya uchumi na maendeleo.

Chama hicho pia kimeeleza ushindi wake ilioupata katika uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye Kata 47 Tanzania Bara uliofanyika Desemba 2, 2018.

Amesema CCM  imepita bila kupingwa katika Kata 41 na katika Kata 6 ambako kumefanyika uchaguzi chama hicho kimeshinda kwa kishindo.

Desemba 17 na 18, 2018 jijini Dar es Salaam chama hicho kitakuwa na kikao cha kawaida cha uongozi wa Taifa.

Amefafanua kuwa Desemba 17, kitakuwa na kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa huku Desemba 18, kitafanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.