Chadema waonja joto la mikutano ya ndani

Muktasari:

  • Viongozi wakuu wa chama hicho wamekamatwa mara mbili katika siku za karibuni wakijiandaa kwa ajili ya mikutano yao ya ndani, polisi wamezungumzia pia ushirikiano wao na wanasiasa

Dar es Salaam. Viongozi wa Chadema wameonja joto la Polisi katika mikoa ya Iringa na Kilimanjaro walikokusudia kufanya mikutano ya ndani, lakini wakaishia kukamatwa.

Hali hiyo ilijitokeza siku chache zilizopita baada ya jeshi hilo kuzuia mikutano yao na kisha kuwakamata viongozi wa chama hicho waliopaswa kuiendesha.

Mkoani Iringa, Desemba 16, mwaka jana, Polisi walimkamata Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu akiwa anajiandaa kushiriki kikao cha ndani mjini Mafinga wilayani Mufindi.

Siku tatu zilizopita, Polisi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro walizuia mkutano wa ndani na kisha kuwakamata viongozi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji na wenzake watatu kwa madai ya kufanya mkusanyiko usiokuwa halali kisheria.

Septemba 22, 2016, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Marijani aliondoa zuio kwa mikutano ya ndani ya vyama vya siasa kwa madai kuwa jeshi hilo limeridhishwa na hali ya kiusalama iliyopo nchini.

Kwa mujibu wa Dk Mashinji, kukamatwa kwa viongozi hao kumefanyika wakati Chadema ikiendesha mikutano ya ndani katika mikoa mbalimbali na kanda za chama hicho.

Alisema lengo lao ni kufanya tathmini na kutoa maelekezo kwa watendaji wao kujiandaa na uchaguzi wa viongozi wa Taifa utakaofanyika Septemba mwaka huu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi alipoulizwa kuhusu mikutano ya ndani ya vyama isiyohitaji vibali, alisema linaweza kuwapo zuio kulingana na mazingira ya mikutano husika.

“Kamanda wa Polisi Kilimanjaro umezungumza naye? atakwambia ni mazingira gani, pia wa Iringa mpigie atakupa mazingira gani yaliyosababisha, mie sijui ni mazingira gani hata mimi naweza kukamatwa endapo nitafanya kitu ambacho kiko kinyume na utaratibu, sasa sijui mazingira gani yalisababisha wao wakamatwe,” alisema Msangi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema hakuna zuio la mikutano ya ndani kwa vyama vya siasa mkoani humo.

Alisema mkoa huo umetawaliwa na Chadema na wamekuwa wakishirikiana nao katika maeneo mengi, lakini alilalamikia mitandao ya kijamii kuwa inaeneza upotoshaji na uchonganishi dhidi ya Polisi na chama hicho.

Alipoulizwa kuna kosa lolote kama chama hakitatoa taarifa ya mkutano wake kwa Polisi, Kamanda Issah alisema mazingira ya sasa yanawalazimu kutoa taarifa ili kulinda usalama wao.

“Kwa hali ilivyo tete sasa hivi watu wanavyozusha mambo, mara wanasema watu wametekwa na watu wasiojulikana, ni vizuri vyombo vya usalama vikawaangalia, hatutawafuata kwenye mikutano yao, lakini ni vizuri wakapita tu wakasema mtuangalie tuko sehemu fulani, tujue mkutano angalau tuwe na ABC ya kuwaangalia, cha msingi ni maridhiano tu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho waliokuwa wakijiandaa kwa mkutano wa ndani, aliomba kutafutwa baadaye baada ya kumaliza mkutano. Hata hivyo, baadaye alipotafutwa hakupatikana.

Akiwa Ikulu Juni 23, 2016, Rais John Magufuli alipiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa hadi 2020, isipokuwa kwa wabunge na madiwani kuifanyia katika maeneo wanayoyayawakilisha bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani ili kutoa fursa kwa Serikali yake kutekeleza waliyoyaahidi kwa wananchi 2015.