Chadema wazungumzia kukamatwa kwa Salum Mwalimu

Dar es Salaam. Polisi mjini Mafinga mkoani Iringa jana ilimkamata naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu wakati akijiandaa kushiriki kikao cha ndani cha chama hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alipotafutwa jana jioni kutolea ufafanuzi tukio hilo alisema yupo kikaoni huku mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William simu yake ya mkononi ikiita bila majibu.

Habari kutoka mjini humo zilisema mwanasiasa huyo alikamatwa na kuachiwa jioni, lakini alitakiwa kuripoti polisi leo.

Akizungumzia kukamatwa kwa Mwalimu, ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene alisema kabla hajakamatwa polisi saba walimshusha kwenye gari.

Makene alisema awali takribani polisi 10 walifika katika ukumbi wa Mamu mjini humo aliotakiwa kufanyia mkutano na kukuta maandalizi yakiendelea, kisha waliagiza usifanyike kwa maelezo kuwa wameagizwa na William.

“Alikamatwa akiwa anaelekea kwenye kikao cha ndani Mafinga akitokea Kanda ya Nyasa kama mnavyojua tunaendelea na programu ya ujenzi wa chama ikiwemo ya Chadema ni msingi,” alisema.

Alisema mbali na Mwalimu wengine waliokamatwa ni katibu wa Chadema Mkoa wa Iringa, Jackson Mnyawami na mwenyekiti wa Bavicha Mbeya Mjini, Jailos Mwaijande.

“Polisi watoe taarifa ya tukio hili kuhusu kukamatwa kwa Mwalimu na viongozi wengine na kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa mujibu kwa sheria.”

Jana jioni mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wametuma wanasheria wao Mafinga ili kushughulikia suala hilo.

“Tumetuma timu yetu kwa ajili ya kuhakikisha Mwalimu na viongozi wengine aliokamatwa nao wanapata dhamana na kuachiwa,” alisema.