Chuo cha Aga Khan wajadili afya ya wanawake EAC

Washiriki  wa Kongamano la kujadili afya za akina mama wa Jumuia ya Afrika Mashariki na changamoto zinazowakabili lililoanza jana jijini Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Wadau mbalimbali wakiwamo wa sekta ya afya na maendeleo wamekutana katika kongamano la kujadili afya ya wanawake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Hospitali ya Aga Khan na Chuo Kikuu cha Udaktari Bingwa cha Aga Khan, wamefanya kongamano kujadili afya za wanawake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Kongamano hilo la siku mbili lililoanza leo, Alhamisi, Desemba 6, 2018 pamoja na kujadili suala la afya za kina mama pia, watajadili changamoto zinazowakabili, ambapo watu wa kada mbalimbali wamehudhuria.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Udaktari Bingwa cha Aga Khan tawi la Dar es Salaam, Profesa Hussein Kidanto amesema kongamano hilo linafanyika ikizingatiwa kuwa Tanzania bado haijafanya vizuri kwenye malengo ya milenia kwenye sekta ya afya.

Amesema tatizo la vifo vya kina mama na mimba za utotoni  nchini ndiyo sababu zilizowafanya kuandaa kongamano hilo kwa ajili ya kujadili hali hiyo.

“Afya ya mama na mimba za utotoni bado ni tatizo, ndio maana tupo hapa. Pia tumemwalika kaimu mkurugenzi wa idara ya watoto na vijana ili tujadiliane  namna ya kupunguza matatizo haya,” amesema Profesa Kidanto.

Amesema mapendekezo na maoni yatakayotolewa katika kongamano hilo yatapelekwa serikalini kwa ajili ya hatua za utekelezaji na kukabiliana na changamoto hizo.

Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Aga Khan, Lucy Ngwai amesema majadiliano hayo yatawasaidia kutengeneza mbinu na mkakati utakaosaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Makuwami Mohamed amekipongeza Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kuzalisha madaktari wanaotoa mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini.