Chuo cha TIPM chawakumbuka wenye uhitaji

Muktasari:

  • Chuo cha Usimamizi wa Miradi Tanzania (TIPM) kimeazimisha siku ya mahafali kwa kuchangia damu kama sehemu ya msaada ndani ya jamii hasa yenye uhitaji ikiwamo wagonjwa.

Dar es Salaam. Chuo cha Usimamizi wa Miradi Tanzania (TIPM) kimeadhimisha siku ya mahafali kwa kuchangia damu kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katikaTaasisi ya Saratani ya Ocean Road ikiwa ni sehemu ya kusadia jamii zenye uhitaji.

Mbali na kuchangia damu chuo hicho, kimewapatia wagonjwa hao misaada mbalimbali ya nguo, matunda, pempasi, sabuni na mafuta ya kupaka.

Akizunngumza baada ya kukabidhi misaada hiyo leo Jumamosi Novemba 17, 2018 mkurugenzi wa TIPM, Lwitiko Mwalukasa amesema moja ya mafanikio ya taasisi au shirika lolote ni kusaidia wagonjwa au watu wengine wenye uhitaji.

"Siku hii ni maalumu kwa ajili ya kusaidia jamii hii ambayo ina uhitaji kwa hiyo tumeona kuliko kutumia fedha kwa ajili ya kufanya mambo mengi ni bora kusaidia hawa wenzetu ambao wanahitaji msaada hasa damu," amasema.

Amesema katika vitu muhimu ambavyo wagonjwa wa saratani wanahitaji mara kwa mara ni damu, hivyo lengo ni kuona msaada huo unakuwa sehemu ya kufanikisha matibabu ya wagonjwa hao.

"Tumeona tatizo hili la saratani lina uhitaji mkubwa wa damu, kwa hiyo  hilo ndiyo lengo letu lililotuleta hapa tupo na jumuiya nzima ya wanataaluma na wafanyakazi ikiwa ni moja ya kuadhimisha siku ya mahafali yetu ya tatu," ameongeza.

Naye mkurugenzi wa tiba na huduma shirikishi Ocean Road, Yokebeth Vuhahola ameomba taasisi nyingine kujitolea kusaidia wangonjwa hasa kuchangia damu.

"Tunashukuru sana kwa msaada huu ambao kwetu sisi ni mkubwa sana, lakini mashirika au taasisi nyingine zisisite kutusaidia kwani bila misaada hatuwezi kutatua changamoto mbalimbali," amesema.