Congo wataka kununua mahindi ya Tanzania

Muktasari:

Kama wewe ni mkulima wa mahindi na upo Mtwara unapaswa kucheka tu kutokana na wafanyabiashara wa mahindi wa Tanzania kutakiwa kuchangamkia soko la mahindi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa mahindi wa Tanzania wametakiwa kuchangamkia soko la mahindi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Taarifa ya ubalozi wa Tanzania nchini Congo iliyotolewa leo imeeleza kuna mahitaji makubwa ya mahindi katika jimbo ya Haut- Katanga na Tanganyika nchini humo.

Taarifa hiyo iliyopitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, imeutaka uongozi wa mkoa huo kuwajulisha wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia soko hilo.

Katibu tawala wa Mkoa wa Mtwara, Jilly Maleko amethibitisha kupokea barua ya Tamisemi na kukiandikia barua Chama cha Wamiliki wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) Novemba 2 kuhusu fursa hiyo.

“Tamisemi ndiyo waliotupa taarifa ili tuwajulishe wadau. Wadau wetu kwa Mtwara ni TCCIA Mtwara,” amesema Maleko.