DC Dodoma ataka mitaa ipewe majina ya wasanii, wachezaji

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amesema moja ya njia ya kuwathamini wachezaji na wasanii maarufu Tanzania ni kutenga mitaa na barabara zitakazopewa majina yao

Dodoma. Wakazi wa jijini Dodoma wametakiwa kutenga baadhi ya mitaa na barabara ili kupewa majina ya wachezaji na wasanii maarufu nchini Tanzania kama njia moja ya kuwakumbuka.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Desemba 12, 2018 na mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi wakati akifungua mkutano wa wadau wa Anuani za Makazi na Postikodi.

Mbali na makundi hayo, amesema wafanyabiashara wanaweza kuinunua mitaa na kuipa majina yao na kwamba watakuwa wakilipia kama ambavyo hufanya watu wanaoandika majina yao katika namba za magari.

Katambi amesema heshima kwa wachezaji na wasanii wanaotamba inaweza kuwekwa kwa kuwatambua katika mitaa na itawafanya wajisikie wanathaminiwa.

 

“Kwa upande wa matajiri sina maana mnunue mitaa iwe mali yenu lakini mnaweza kuomba mtaa fulani ukaitwa kwa jina lako halafu mwisho wa siku tukakubaliana ukawa unalipa kiasi fulani cha fedha kwa mwaka,” amesema.

 

Katambi pia amezungumzia leseni za biashara akiwataka wafanyabiashara watakaoomba leseni hizo kutopatiwa kama mitaa wanayotoka haina Postikodi kwa maelezo kuwa Serikali inataka kuwatambua katika ulipaji wa mapato na masuala ya usalama.