DC Jerry Muro ampongeza Magufuli kuwateua vijana

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha,Jerry Muro akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa mwaka wa vijana katika nchi za Afrika Mashariki uliofanyika katika taasisi ya MS TCDC leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha, Jerry Muro amesema vijana waliopewa dhamana katika utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli wafanye kazi ili wasimwangushe

Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Jerry Muro amesema Serikali ya Tanzania imepiga hatua katika kuwawezesha vijana kwa kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.

Muro amesema hayo leo Jumatatu Novemba 19, 2018 wakati akitoa salamu za Serikali kwenye mkutano wa pili wa mwaka wa vijana katika nchi za Afrika Mashariki unaofanyika katika kituo cha MS TCDC.

"Rais John Magufuli ameonyesha imani kubwa kwa kuwaamini vijana na amewateua kushika nyadhifa zikiwemo mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya," amesema Muro.

Muro hata hivyo, amekemea tabia ya vijana kutumia teknolojia ya mawasiliano vibaya kwa kuweka picha zisizo na maadili badala ya kuchangamkia fursa hiyo kutangaza biashara na kazi za ubunifu.