DC Katambi amlaza mahabusu diwani wa CCM

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amemuweka mahabusu diwani wa Chang'ombe kupitia CCM jijini Dodoma akimtuhumu kusababisha migogoro ya ardhi.


Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambo amemlaza mahabusu Diwani wa Chang'ombe (CCM), Bakari Fundikira akimtuhumu kuchochea migogoro ya ardhi katika eneo lake.

Diwani huyo alikamatwa jana asubuhi Jumatano Januari 9, 2019 na kupelekwa Kituo Kikuu cha Dodoma ambapo mpaka saa 6 asubuhi leo, alikuwa hajatoka na utaratibu wa kumuwekea dhamana ulikuwa unaendelea.

Taarifa za kukamatwa kwa diwani huyo zilikuwa za siri kwa baadhi ya viongozi kukataa kuzungumzia jambo hilo, hata hivyo mmoja wa madiwani kata za jirani na kata hiyo alidokeza juu ya ukweli huo.

"Ni kweli diwani mwenzetu anashikiliwa na polisi kwa agizo la mkuu wa wilaya, lakini naamini ni mambo madogo ambayo hayakupaswa kufika huko,"amesema mmoja wa madiwani wa Jiji aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ya mkononi, Katambi aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), haikupokewa lakini baadaye alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi kukiri kumuweka ndani diwani huyo.