DC Mwanga aagiza ofisa ‘Usalama wa Taifa’ kujisalimisha

Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho

Muktasari:

  • DC ametoa agizo la kukamatwa kwa mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni ofisa usalama wa Taifa, baada ya wavuvi kudai alifika kijijini na kuwachangisha fedha ili kumhonga mkuu wa wilaya.

Mwanga. Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho, ametoa saa 48 kwa mtu anayejifanya ni ofisa wa Usalama wa Taifa na kuwatapeli wavuvi katika bwawa la Nyumba ya Mungu kujisalimisha polisi.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo jana Desemba 9,2018 katika kijiji cha Lang’ata Bora, alipokwenda kwa ajili ya kazi ya kuteketeza zana za uvuvi haramu zilizokamatwa kijijini hapo.

Agizo la Mbogho linatokana na malalamiko ya wananchi kuwa mtu huyo amekusanya fedha kwa wavuvi akisema anazipeleka kwa mkuu huyo wa wilaya ili kulegeza operesheni dhidi ya uvuvi haramu.

Wavuvi katika kijiji hicho walimweleza mkuu wa wilaya kuwa mtu huyo anayejiita Sajo alichukua fedha hizo akidai anazipeleka kwake ili awaruhusu kuvua katika mwalo mdogo uliozuiwa.

Mmoja wa wavuvi hao, Samwel Kifoyo amedai kuwa mtu huyo aliwahi kujishughulisha na ununuzi wa samaki kijijini hapo siku za nyuma, lakini amerudi na kudai ni ofisa usalama wa Taifa.

Akijibu malalamiko hayo, Mbogho amesema hakuna ofisa usalama wa Taifa anayeweza kujiingiza katika vitendo vya aina hiyo hivyo, kumtaka hadi kufikia kesho awe amejisalimisha polisi.

“Na nyinyi wavuvi acheni kulegeza akili yenu. Mnaambiwaje mtoe fedha ili kumuona mkuu wa wilaya na nyinyi mnatoa. Huyo anayejiita usalama wa Taifa hawezi kuwa afisa Usalama,” alieleza.

Mbogho alimpa mtu huyo hadi kesho Jumanne, awe ameripoti mwenyewe kwa mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) wa wilaya ya Mwanga.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, endapo atakaidi kujisalimisha mwenyewe akiwa na fedha alizokusanya kutoka kwa wavuvi, serikali itatumia nguvu kumsakama na asije akajilaumu.