Dk Abbas asema wanahabari wana haki ya kuikosoa Serikali

Muktasari:

Waandishi wa Habari nchini  Tanzania  wana haki ya kuikosoa Serikali na  sekta binafsi, lakini hawapaswi kuandika habari za kuzusha na kupotosha jamii na kusababisha uvunjifu wa amani.


Dar es Salaam. Waandishi wa Habari nchini  Tanzania  wana haki ya kuikosoa Serikali na  sekta binafsi, lakini hawapaswi kuandika habari za kuzusha na kupotosha jamii na kusababisha uvunjifu wa amani.

Hayo yameelezewa leo Jumamosi Desemba 22, 2018 na Msemaji  wa Serikali, Dk Hassan Abbas katika warsha ya waandishi wa habari kuhusu jukumu lao katika kutoa habari iliyoandaliwa na Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (TIC).

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano iliyojikita katika kupambana na rushwa na utoaji huduma bora kwa jamii inahitaji waandishi wanaokosoa kwa haki na kwa utafiti ili kuonesha maeneo ambako watendaji wanakosea au wanakwaza utekelezaji.

Amesema lengo ni ili wachukuliwe hatua lakini badala yake amedai wanahabari wengi wanajikita katika habari za siasa, na uzushi ambazo hazina tija kwa jamii.

Amesema mwandishi aliyefanya utafiti vizuri na kubaini madudu ndani ya Serikali na akawa na uthibitisho sahihi ana uwezo wa kuandika habari na kuichapisha kwenye vyombo vya habari.

Amesema Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kifungu cha 52 (2) kinatoa haki hiyo ya kila mwandishi kuikosoa Serikali na kwamba kifungu cha 52 kinaeleza haitakuwa kosa kwa waandishi watakaoonyesha makosa serikalini na si kuzusha au kuandika habari za chuki.

"Kwa mara ya kwanza Tanzania tumeweka kifungu hicho cha sheria ili kutoa haki ya kitaaluma kwa waandishi wa habari ambao ndio mhimili wa nne wa nchi, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kukosoa kistaha na sio kutukana wala kukashifu mtu au taasisi fulani," amesema Dk Abbas.

"Wakati mwingine  tunapochukua hatua kali ya kulifungia gazeti au chombo cha habari kwa kuwa na habari zenye kuhatarisha usalama wa nchi, wanaharakati wengi wanalalamikia hatua hizo. Tunasahau waandishi pamoja na kuwa na haki wana wajibu wa kulinda nchi," amesema Dk Abbas.

Amebainisha mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia unaeleza haki na wajibu wa kitaaluma pamoja na mipaka yake.

Awali, kiongozi mkuu wa dhehebu hilo, Sheikh Hemed Jalala amesema wajibu wa mwandishi wa habari ni kuandika habari zenye kufuata misingi ya haki na sheria.

"Mwandishi wa habari mzalendo ni yule anayeitakia jamii isonge mbele kwa kuenzi mambo mazuri badala ya kuandika habari zinazofitinisha au  kuchochea jambo ambalo  litaleta chuki baina ya jamii moja na nyingine," amesema Jalala.

Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) , Edda Sanga anasema bado vyombo vya habari havitoi fursa ipasavyo kwa wanahabari wanawake katika nafasi za juu za uongozi .

"Nilipongeze gazeti la Mwananchi kwa kuwapa uongozi wa juu waandishi wa habari wanawake," amesema  Edda

"Kwa mfano, mwaka 2008 ni wanawake watatu pekee ndio walishinda kwenye Tuzo za Umahiri wa habari (EJAT) zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Walishinda uandishi wa habari za uchunguzi," anasema Sanga.