Dk Bashiru agoma kumzungumzia Membe

Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ali 

Muktasari:

Jana Jumanne Desemba 18, 2018 Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kimewasamehe na kuwarejeshea uanachama  waliokuwa wenyeviti wa mikoa wa chama hicho huku kikimpitisha Abdallah Mtolea kuwania ubunge wa Temeke. Awali Mtolea alikuwa mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF

Dar es Salaam. Wakati CCM ikiwasamehe na kuwarejeshea uanachama wenyeviti wa zamani waliowahi kuongoza mikoa mitatu na wilaya moja, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally amegoma kuzungumzia sakata la waziri wa zamani, Bernard Membe.

Akitangaza msamaha dhidi ya wanachama hao mbele ya wanahabari jana, Dk Bashiru alikataa kujibu swali lolote lililomhusisha Membe.

Hivi karibuni, katibu mkuu huyo wa chama tawala aliibua mjadala nchini pale alipomtaka Membe, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne afike ofisini kwake kujibu madai kuwa amekuwa akitajwa kutaka kumkwamisha Rais John Magufuli. Hata hivyo, jana baada ya kumaliza kusoma maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wanahabari walitaka kujua mwendelezo wa suala la Membe, lakini kiongozi huyo alikataa kujibu chochote akitaka atafutwe wakati mwingine.

Urejeshwaji wanachama

Wanachama waliorejeshewa uanachama baada ya kufukuzwa ni waliokuwa wenyeviti wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida; Erasto Kwirasa (Shinyanga), Christopher Sanya (Mara) na Salum Madenge (Kinondoni).

Dk Bashiru alisema msamaha huo ni sehemu ya maazimio ya kikao hicho kilichokutana jana asubuni Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilichoongozwa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kilikutana kwa ajili ya kupokea taarifa kuhusu masuala ya maadili na utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa Zanzibar na Tanzania Bara.

Dk Bashiru alisema kiliridhia pia uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa CCM na marekebisho ya kanuni za fedha, mali za chama na jumuiya zake.

Vilevile, alisema NEC imetupilia mbali mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa kwa viongozi wanne wa chama hicho akiwamo mwenyekiti wa Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo.

“NEC imepitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama katika ngazi za wilaya, mkoa na Taifa zilizoachwa wazi. Pia imetoa adhabu ya karipio kwa mwanachama wa CCM, Hasnain Murji kutokana na makosa ya kimaadili,” alisema Dk Bashiru. Hata hivyo, kikao hicho kimemuweka chini ya uangalizi usiokuwa na kikomo mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu aliyeomba kurejeshewa uanachama. Jesca alifukuzwa kwa makosa ya kimaadili.

Dk Bashiru alisema kikao hicho pia kimempitisha Abdallah Mtolea kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa marudio Jimbo la Temeke. Mtolea alihamia CCM akitokea CUF alikokuwa mbunge wa jimbo hilo.

Katika hatua nyingine, alikanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni kuhusu kuondolewa kikaoni kwa mjumbe wa NEC, Stephen Wasira.

Awali taarifa zilizosambaa mitandaoni zilisema mwanasiasa huyo mkongwe aliondolewa kwa madai kuwa alitaka kupinga kufukuzwa Membe uanachama.