Dk Bashiru ataja korosho akimshukia tena Membe

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally .

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekosoa kauli ya Bernard Membe kuwa yeye ni mgeni ndani ya chama tawala, kubainisha kuwa anataka kuonana na waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya kuchota busara zake kuhusu zao la korosho

Geita. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekosoa kauli iliyotolewa na Bernard Membe aliyedai kuwa msomi huyo ni mgeni ndani ya chama tawala, kusisitiza kuwa anataka kuonana naye ili achote busara za waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu zao la korosho

Katika maelezo yake Dk Bashiru amesema yeye ni mgeni katika timu Membe na timu ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini si mgeni kwenye kanuni za CCM.

Bashiru ametoa kauli hiyo jana usiku Desemba 2, 2018 mjini Geita baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita.

Kauli hiyo ya Dk Bashiru ni mwendelezo wa vita yake na Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akimtaka afike ofisini kwake kujieleza.

Alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza akiwa mkoani Geita, akijibu ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya mtandaoni ya mtu mwenye jina la Bernard Membe kujibu tuhuma zilizotolewa na Dk Bashiru akiwa Geita.

Dk Bashiru alimtuhumu Membe kuandaa mpango wa kumkwamisha Rais John Magufuli katika uchaguzi wa rais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana na mbunge huyo za zamani wa Mtama.

Membe alieleza kushangazwa na utaratibu uliotumika kumuita akibainisha kuwa pengine ni ugeni wa kazini wa Bashiru, lakini akaahidi kwenda kumuona akirudi safari ya nje ya nchi.

Lakini jana katika majibu yake Dk Bashiru ameonekana kukerwa na kauli kuwa yeye ni mgeni kazini.

Dk Bashiru amesema tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amekutana na wanachama wengi, akiwemo mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) na kwamba wito wake kwa Membe ni kawaida na ni taratibu za CCM.

Pia, amesisitiza Membe kwenda kumuona ili ampe busara na si mashtaka.

“Mimi simuhitaji kwa mashtaka nahitaji busara zake alikuwa mbunge kule Mtama sasa tunahangaika na korosho tunapambana na Kangomba ambayo inahusisha viongozi wa chama na Serikali,  aje anipe busara tunataka kutokomeza unyonyaji kwa wakulima aje anipe busara,” amesema Bashiru.

Amesema hamzuii Membe kumjibu kwenye mitandao ya kijamii lakini majibu anayotoa yatatoa nafasi kwenye chama kumpima.

Bashiru amesema hawezi kumzungumzia mtu aliyetoa tuhuma dhidi ya Membe kwa kuwa CCM si chama cha kuzungumzia wanaharakati.

Dk Bashiru alisema wanafanya mageuzi makubwa kwenye chama kuhusu tabia hivyo wanaokosoa waendelee kukosoa lakini yeye anafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama na sio mitandao ya kijamii.