Dk Bashiru awapatanisha Diallo, Mecky Sadik

Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Mwanza Antony Dialo akishikana Mkono na aliyekuwa mgombea mwenza wa wenyekiti Na Mkuu wa Mkoa ya Dsm na Kilimanjaro Said Mecky Sadik

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaagiza mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo na aliyekuwa mshindani wake kwenye uchaguzi ndani ya chama mwaka 2017, Mecky Sadik kumaliza tofauti zao na kuungana kukijenga chama hicho na kuisimamia Serikali.

Mwanza. Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally amemaliza mgogoro wa mchakato wa uchaguzi uliodumu kati ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani Mwanza, Dk Anthony Diallo na aliyekuwa mshindani wake wakati wa uchaguzi, Mecky Sadik.

Tangu kumalizika uchaguzi ndani ya chama hicho tawala mwaka 2017, vigogo hao na makundi yanayowaunga mkono wamekuwa wakisigana huku kila upande ukuutuhumu upande mwingine kwa hujuma.

Akitangaza kuhitimisha mgogoro huo kwa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza leo Jumanne Januari 8, 2019, Dk Bashiru amewaagiza viongozi na wana CCM mkoani humo kusahahu yaliyotokea wakati wa mchakato na uchaguzi ndani ya chama na kujielekeza katika ujenzi wa chama na kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

“Baada ya kupokea, kuyachunguza na kuyafanyia kazi malalamiko ya ndugu Mecky Sadik, vikao vya maamuzi vimeamua kuwa aliyeshinda aachwe afanye kazi na aliyeshindwa aungane naye kufanya kazi ya kukijenga chama,” alisema Dk Bashiru.

“Huo ndio msimamo wa chama. Kilichobaki ni wote (Diallo na Sadik) kushirikiana kwa pamoja kujenga chama,” ameongeza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kauli ya Dk Bashiri, Dk Diallo na Sadik wote wametangaza kukubaliana na maamuzi ya vikao vya chama na kuahidi kushirikiana kukijenga chama hicho.

“Nakubaliana na maamuzi na maelekezo ya chama. Nitashirikiana na mwenyekiti wangu wa mkoa (Dk Diallo) kukijenga chama, lakini ni rai yangu kuwa kamati ya siasa na halmashauri ya mkoa zihakikishe zinatenda haki kwa wagombea wote kwenye mchakato wa chaguzi ndani ya chama,” amesema Sadik aliyewahi kuwa mkuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro

Dk Diallo naye alisema hana kinyongo wala mgogoro na Sadik huku akielekeza lawama kwa wapambe aliosema ndio walikuwa wakiwagombanisha.

Vigogo hao wawili walichuana vikali kuwania uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza huku Dk Diallo akiandamwa na matukio ya yeye mwenyewe gari lake kupekuliwa na maofisa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Sengerema.