Dk Kigwangalla asema maambukizi ya malaria yamepungua

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangala akizungumza bungeni wakati akijibu maswali ya wabunge kwa niaba ya Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Maralia imepungua nchini Tanzania kwa asilimia 50 kutoka asilimia 18.1 hadi asilimia 7.3

Dodoma. Maambukizi ya malaria yamepungua nchini kutoka asilimia 18.1 (2008) hadi kufikia asilimia 7.3 kwa mwaka 2017.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ameliambia Bunge leo Ijumaa Novemba 16, 2018 wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambaye hakuwepo bungeni.

Dk Kigwangalla amesema juhudi zinazofanyika katika kudhibiti malaria zimezaa matunda kwa kiwango cha kupungua kwa asilimia 50.

Katika swali la msingi Mbunge wa Kibaha (CCM), Silvestry Koka ametaka kujua Serikali ina mkakati gani kukamilisha azma ya kupunguza malaria nchini.

Akijibu swali hilo, Waziri Kigwangalla amesema Serikali ina dhamira na nia ya kutokomeza magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa malaria.

"Serikali imeendelea kutekeleza mikakati muhimu ya kudhibiti malaria, ambayo imependekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)," amesema Dk Kigwangala

Amesema ili kufikia lengo la kupunguza maambukizi katika jamii na hatimaye kutokomeza malaria nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau inatekeleza afua mbalimbali za kinga na tiba.

Amezitaja afua hizo kuwa ni pamoja na kugawa vyandarua vyenye dawa (LLINs) bila malipo ili kuwakinga watu kuumwa na mbu, kupulizia viuatilifu ukoko ndani ya nyumba na kuangamiza viluwiluwi wa mbu.