Dodoma ina uhaba wa walimu 12,454 wa shule za msingi

Muktasari:

Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari ikielezwa kuwa una walimu wa masomo hayo 959 kati ya 1,396 wanaohitajika

Dodoma. Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari ikielezwa kuwa una walimu wa masomo hayo 959 kati ya 1,396 wanaohitajika.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Dodoma (RCC), ofisa elimu taaluma Mkoa wa Dodoma, Eliud Njogellah amesema kuwa upungufu huo ni sawa na asilimia 31 huku walimu wa masomo ya sanaa wakiwa 2,481 na ziada ya walimu 569.

Amesema mpaka sasa mkoa huu unahitaji walimu 12,454 kwa shule za msingi, kwamba waliopo ni walimu 7,582 tu huku maeneo ya pembezoni mwa mji yakiwa na uhitaji mkubwa wa walimu kuliko yale ya mijini.

Kwa upande wa vyumba vya madarasa, Njogellah amesema mahitaji ni vyumba 12,671 lakini vilivyopo ni 6,093.

Kwa upande wa madawati amesema  yanayohitajika ni 167,673 na yaliyopo ni 129,754 na kusisitiza kuwa uhaba huo umetokana na mpango wa serikali kutoa elimu bila malipo.

Kwa upande wa shule za sekondari amesema wanafunzi 5,991 wameshindwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019  kutokana na kukosa vyumba vya madarasa.

"Tunahitaji jumla ya vyumba vya madarasa 120 ili hawa wanafunzi waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza waendelee na masomo ifikapo Januari. Halmashauri husika  naomba zifanye juhudi za kutosha,” amesema.

Hata hivyo naibu Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Ashatu Kijaji amewataka watumishi waliopewa dhamana katika Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanabeba dhamana ya kutatua changamoto za elimu ili kuongeza alama za ufaulu kwa wanafunzi.