Friday, November 8, 2013

Ekelege kizimbani

By Tausi Ally, Mwanachi

Dar es Salaam.Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Wakala wa Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwaondolea ada ya asilimia 50 Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors.

Akisomea hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Janeth Machulya alidai Machi 28, 2008 mshtakiwa akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS kwa nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kuziondolea kampuni hizo ada yenye thamani ya Dola 42,543 za Marekani (Sh68,068,800).

Machulya alidai mshtakiwa aliziondolea ada kampuni hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS.

Katika shtaka la pili, anadaiwa kutokana na kitendo hicho mshtakiwa alisababisha hasara ya Dola 42,543 za Marekani.

Mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika na kuomba mahakama ipange tarehe ya usikilizaji maelezo ya awali (PH).

Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12, mwaka huu mshtakiwa atakaposomewa maelezo ya awali, aliachiwa huru kwa dhamana ya Sh35 milioni.

Wakati huohuo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Togolai Kimweri anayekabiliwa na mashtaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi na mwenzake, ameieleza Mahakama kuwa Kurugenzi ya Usalama Ikulu, iliridhia ujenzi wa ghorofa 18 na kuomba sehemu ya juu wapewe wao.

Togolai aliyaeleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo alipoongozwa na Wakili Richard Rweyongeza kujitetea dhidi ya mashtaka hayo yanayomkabili. Alidai ujenzi ulifuata taratibu zote na kwamba, anahisi kushtakiwa kwake kumetokana na kashfa aliyowahi kuipata Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli iliyowahi kuripotiwa katika vyombo vya habari.

Aliendelea kueleza kuwa jengo hilo serikali inapata asilimia 25 na mwekezaji anapata asilimia 75 mwekezaji na kwamba hajawahi kutoa hati ya viwanja namba 45na 46 vilivyopo mtaa wa Chimara kwa mwekezaji ili apate mkopo.

Alidai kuwa madai hayo ni ya uongo na kwamba hati haijawahi kutoka hadi sasa ipo TBA na kwamba iwapo viwanja hivyo vingeuzwa wakati huo vingeuzwa kwa Sh 1.30 bilioni na sasa thamani hiyo inazidi Sh 9.8 bilioni.

Aliongeza kuwa wakati ujenzi wa jengo hilo ulipofikia gorofa ya 15, aliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama na wakampelekea na mchoro ambao aliupitia na kuwataka waendelee hadi gorofa ya 18 kama ilivyopangwa ila sehemu ya Juu wapewe usalama.

Alidai kuwa baadaye walipokea barua toka kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Philimon Luhanjo ikizungumzia kuhusu makubaliano hayo na kwamba hajawahi kupata malalamiko yoyote kuhusiana na ujenzi huo.

“Rais alipewa taarifa ya utendaji wa TBA kuhusu mradi huo na kamba katika vikao vya bajeti vya bunge vya 2007/2008 na 2008/2009 mradi huo ulitolewa taarifa zake bungeni katika hotuba ya John Magufuli na Shukuru Kawambwa.”Alidai shahidi huyo wa utetezi.

Alisisitiza kuwa taarifa zote kuhusu mradi huo zilikuwa zikitolewa Wizarani, yeye hakuwa mjumbe wa bodi, bodi ndiyo ilikuwa na uwezo wa kuupitisha huo mradi ama kuukataa na kwamba wazo lilikuwa mradi wa ujenzi wa gorofa sita lakini rasimu ya mkataba iliandaliwa na kupelekwa kwa AG pamoja na mkataba unazungumzia gorofa 15 hadi 25.

Aliiomba mahakama kuifuta kesi hiyo na mashtaka yanayowakabili yeye na mwenzake kwa sababu alikuwa akihakikisha anafanya kazi kulingana na maelekezo ya sharia ya wakala.

Mbali na Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Kimweri mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Msanifu Mkuu wake, Richard Maliyaga.

Awali upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Leonard Swai, ukitoa ushahidi katika kesi hiyo, uliwaita jumla ya mashahidi 13 pamoja na vielelezo 20 na baada ya mashahidi hao kutoa ushahidi wao mahakama iliwaona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu na kuwataka kuanza kujitetea.

Washtakiwa Kimweri na Maliyaga wanakabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.

Swai akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao, alidai kuwa Agosti 6, mwaka 2007, mikataba miwili kwa ajili ya viwanja namba 45 na 46 washtakiwa hao waliitia saini.

Alidai kuwa katika mkataba huo, upande wa serikali watamiliki asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75 katika jengo la ghorofa 18. Alidai TBA ilitoa vibali vilivyotiwa saini na Maliyaga, kikiwemo cha kuongeza idadi ya ghorofa 15 hadi 18.

Wakili huyo wa Takukuru alidai kuwa eneo hilo lilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa gharofa tatu hadi sita kwa makazi na kwamba washtakiwa hao walitoa kibali kwa mwekezaji bilaya kupata idhidi kutoka kwa mamlaka husika.

-->