Fastjet njia panda, likizembea kidogo leseni kupokwa

Dar es Salaam. Shirika la ndege la Fastjet Tanzania limebakiza siku 13 kufanya marekebisho ya utendaji na endapo litashindwa litafutiwa leseni.

Siku za hivi karibuni shirika hilo ambalo linajinasibu kwa kutoa usafiri wa gharama nafuu limegubikwa na matukio ya kuahirisha safari zake, jambo ambalo limesababisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kusitisha safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia na Zimbabwe.

Kufuatia hatua hiyo, Desemba 14, shirika hilo liliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter likieleza kusitishwa kwa safari hizo hadi hapo zitakapotangazwa tena.

“Wateja walioathiriwa na kusitishwa kwa safari hizi watarudishiwa gharama zao zote kutokana na malipo ya msingi, tunaomba radhi kwa waathirika wote … Safari zote za ndani ya Tanzania zitaendelea kama kawaida,” ulieleza ujumbe huo.

Mmoja wa abiria aliliambia Mwananchi kuwa alikata tiketi ya kwenda Zimbabwe Oktoba 25, lakini Desemba 13 alitumiwa ujumbe akitaarifiwa safari haitakuwepo ikiwa ni siku moja baada ya mumewe kwenda Fastjet na kuthibitisha safari.

Abiria huyo ambaye jina lake tunalihifadhi alieleza kuwa ujumbe huo haukuweka wazi sababu ya kusitishwa kwa safari hiyo zaidi ya kuombwa radhi.

Ujumbe huo ulisomeka, “Ndugu abiria, tunasikitika kukuarifu kuwa safari yako namba 205 ya Desemba 17 kutoka Dar kwenda Harare imesitishwa. Tafadhali wasiliana na ofisi ya Fastjet iliyo karibu nawe au piga simu namba +255784108900. Fastjet inaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.

Mkurugenzi mkuu wa TCAA, Hamza Johari akizungumza na Mwananchi jana, alisema shirika hilo lilipewa siku 28 za kufanya marekebisho ya utendaji wake tangu Desemba 2.

“Kama mamlaka hatutaki shirika ambalo halifanyi biashara vizuri,” alisema.