Fastjet yawaomba radhi abiria kwa kuahirisha safari

Muktasari:

Baada ya abiria waliokuwa wasafiri na ndege ya kampuni ya Fastjet kukwama kutokana na sababu za kiufundi na baadaye safari kuahirishwa, kampuni hiyo imewaomba radhi abiria na kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.


Dar es Salaam. Kampuni ya ndege ya Fastjet imewaomba radhi wateja wake kwa kuahirisha safari kutokana na sababu za kiufundi zilizojitokeza jana Jumatano Desemba 12, 2018 na kusababisha safari kuahirishwa.

Jana kampuni hiyo iliahirisha safari ya kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kuwataka wasafiri waliokuwa waondoke na ndege iliyopangwa kusubiri mpaka leo asubuhi.

 “Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja wetu. Ndege iliyopangwa kusafiri ilipata tatizo la kiufundi hivyo kutulazimu kuahirisha safari,” amesema Lucy Mbogoro, meneja mawasiliano na uhusiano wa Fastjet.

Jana jioni wakati safari inaahirishwa, ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 126 ilikuwa imeandaliwa mpaka asubuhi ya leo abiria hao walitakiwa kupanda ndege nyingine.

Kwa kuwa ndege ya leo asubuhi nayo ilikuwa na abiria, haikuweza kuwabeba abiria wote walioahirishiwa safari na kuilazimu Fastjet kurejesha tiketi zinazowaruhusu abiria kusafiri wakati wowote watakaopenda. Abiria 20 walipewa tiketi hizo.

“Mara nyingi huwa tunawajuza abiria wetu kila inapotokea dharura ya kuahirisha safari. Tunafanya hivyo kwa kuwatumia ujumbe kwenye baruapepe zao au kuwapigia simu,” ameeleza Lucy.

Amesema dharura ikitokea huwafaulisha abiria kwenye ndege za shirika jingine ili kutoathiri mipango yao jambo ambalo halikuwezekana jana jioni kwani ndege za kampuni hizo pia zilikuwa zimejaa.

Hata hivyo, amesema ndege za kampuni nyingine zina uwezo wa kubeba abiria wachache hivyo kuongeza changamoto ya kuwasafirisha wateja hao waliokwama.

Kuahirishwa kwa safari hiyo kulisababisha malalamiko kutoka kwa abiria husika.

Mmoja wao aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Fikiria, unaamka usiku wa manane kuwahi ndege na mnapojiandaa kupanda, mnatangaziwa kuwa ndege imejaa au safari imeahirishwa.”

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema,“Tunachukua hatua dhidi ya Fastjet ili kulinda masilahi ya abiria.”