George H. w. Bush alilazimika kutumia mwamvuli kujiokoa angani

Muktasari:

  • 1966: Alishinda kiti katika Bunge la Wawakilishi
  • 1971: Rais Richard Nixon alimteua kuwa Balozi wa Marekani UN1974: Aliteuliwa kuwa Balozi wa Marekani China
  • 1976: Rais Gerald Ford alimteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la CIA.
  • 1981-1988: Alikuwa Makamu wa Rais Ronald Reagan1989-1893: Aliongoza Marekani akiwa rais wan chi hiyo kwa kipindi kimoja.

Rais wa 41 wa Marekani George Herbert Walker Bush amefariki akiwa na umri wa miaka 94. Wengi wanaweza kumwangalia na kumtambua rais huyo baada ya kuingia katika harakati za kiasa, lakini ukweli ni kwamba ana historia ndefu iliyojaa mitihani, uzalendo kwa taifa lake na mafanikio makubwa.

Bush kabla ya kuwa rais wa 41 wa Marekani na kuongoza kwa awamu moja kuanzia mwaka 1989 hadi 1993, alikuwa ameshaifanyia mambo makubwa nchi yake na kuaminiwa katika nyadhifa mbalimbali nyeti.

Alisajiliwa rasmi na kikosi cha maji cha jeshi la Marekani Juni 13, 1942 baada ya kuhitimu chuo kikuu cha Andover akiwa na umri wa miaka 18 na kuwa rubani mdogo zaidi ndani ya jeshi hilo.

Miezi mitatu baadae alipelekwa bahari ya Pacific kupiga picha baadhi ya maeneo yaliyohusika katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia likiwamo eneo la Midway.

Baada ya mapigano makali kati ya Marekani na Japan katika visiwa vya Marcus na Wake, Bush alishiriki moja kwa moja vita hivyo katika kisiwa cha Marina, Juni mwaka 1944.

Kufanikiwa kwa mapambano katika kisiwa cha Marina, Agosti 1, 1944 Bush alipandishwa cheo na kuwa luteni.

Mwezi mmoja baadae alikabidhiwa jukumu la kurusha ndege vita iliyobeba mabomu kwa ajili ya kukishambulia kituo cha redio cha Japan katika kisiwa cha Chi Chi Jima.

Akitekeleza jukumu hilo, injini ya ndege yake ilishika moto lakini alilazimika kukamilisha mashambulizi. Baadae akisimulia tukio hilo wakati wa uhai wake aliwahi kusema; “Tulifundishwa kukamilisha jukumu bila ya kujali unakumbana na kikwazo gani”.

Wakati akirejea baada ya kuwashinda Wajapan katika vita hivyo, Juni 19 mwaka huo, Bush na wenzake wawili waliruka maili kadhaa na kulazimika kutumia miavuli kujiokoa kutoka kwenye ndege hiyo iliposhika moto.

Hata hivyo, mwenzake mmoja alipoteza maisha baada ya mwamvuli wake kushindwa kufunguka huku mwengine naye akipoteza maisha katika tukio hilo.

Katika moja ya matukio ambayo Bush aliponea kwenye tundu ya sindano ni pale alipotua na ndege yake majini na kulazimika kukaa humo kwa saa nne akiogelea kwa boya huku ndege vita ikimzunguuka hadi alipookolewa na nyambizi ya Marekani ya USS Finback.

Tukio la kuokolewa kwake lilirekodiwa katika mkanda wa video ambao ulitumika mara kwa mara wakati wa kampeni zake za kisiasa kuwania kuingia urais.

Bush aliendelea kukaa ndani ya nyambizi hiyo kwa mwezi mmoja ilipokuwa ikiendelea kutoa msaada kwa wapiganaji wa Marekani katika vita hivyo na kufanikiwa kuwaokoa baadhi ya marubani walionusurika na mashambulizi.

Katika kipindi alichotumika jeshini Bush alirusha ndege vita miruko 58 na kufanikiwa kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu za mashujaa wa Marekani huku akitunukiwa tuzo mbalimbali za ujemedari.

Aingia katika siasa

Bush alistaafu shughuli za kijeshi mwaka 1955 wakati huo akiwa kwenye orodha ya watu waliofanikiwa katika biashara ya mafuta huku akiwa na malengo ya kuwa mwanasiasa.

Bush aliyezaliwa katika jimbo la Massachusetts, Juni 1924 na kukulia Connecticut, aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 1964.

Akiwa na umri wa miaka 40, mwaka 1964 aliingia kwenye rekodi za mamilionea vijana baada ya kupata mafanikio makubwa kupitia biasahara ya mafuta.

Mwaka 1945, Bush alimuoa Barbara Pierce, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18 na kufanikiwa kupata naye watoto sita.

Wamlilia

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May anasema Bush aliongoza kumalizika kwa amani vita baridi na kuifanya dunia kuwa shemu salama kwa kizazi kijacho.

Malkia Elizabeth anasema Bush alikuwa rafiki mwema kwa Uingereza.

Rais wa zamani wa Marekani aliyechukua uongozi mikononi mwa bush baada ya kumshinda katika uchaguzi mkuu, Bill Clinton na mke wake Hillary wanasema utumishi wa muda mrefu wa Bush ulitawaliwa na mapenzi mame na urafiki. “Najivunia kila dakika niliyotumia kuwa naye, milele nitaendelea kuutunza urafiki wetu”.

Kiongozi wa zamani wa kisoviet, Mikhail Gorbachev alimsifu Bush kwa kumaliza vita baridi na kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia.

Mwaka 1991 Bush na Gorbachev walisaini mkataba wa kwanza wa kupunguza matumizi ya makombora ya nyuklia ya masafa marefu.

Mwili wa Bush ulisafirishwa jana kutoka nyumbani kwake Texas alikofariki Ijumaa iliyopita na kupelekwa Washington ambako mazishi yake yatafanyika kesho katika makaburi ya kitaifa, kando mwa kaburi la mkewe aliyefariki na kuzikwa Aprili mwaka huu.

Ameacha watoto watano akiwamo Rais wa 43 wa Marekani, George W Bush ambaye alimuelezea baba yake kuwa mbali na uongozi alikuwa baba bora mwenye upendo, huruma na kujali familia yao.