Hofu yatajwa kuchangia mawaziri kushindwa kuchukua uamuzi

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano,Isaack Kamwele

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi akiwamo Profesa Mohamed Bakar, hofu hiyo inawafanya mawaziri washindwe kujiamini katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kusababisha kutenguliwa au kuachwa.

Dar es Salaam. Isaack Kamwele ameeleza hofu aliyonayo dhidi ya uwezekano wa kuvuliwa uwaziri wakati wowote ule, lakini yawezekana hiyo ndiyo hofu waliyonayo mawaziri wengi.

Na huenda ikawa moja ya sababu za mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kutofanya vizuri na kujikuta wakitumbuliwa, wachambuzi waliohojiwa na Mwananchi wameeleza.

Mwananchi lilitafuta maoni ya wachambuzi hao baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Dk Charles Tizeba, aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Charles Mwijage, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kutokana na kutowajibika ipasavyo katika sakata la mauzo ya korosho na kusababisha Waziri Mkuu na baadaye Rais kuingilia kati kutatua.

Uamuzi huo wa Rais umefanya idadi ya mawaziri alioachana nao tangu aapishwe Novemba 5, 2015 kuzidi nusu ya waliosalia.

“Maana nimesikia Waziri Mkuu akitumwa kwako na Rais, maana yake kuna kitu umeshindwa kufanya. Tusiruhusu hilo likafika, vinginevyo nitang’oka,” alisema Kamwele, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi.

Wachambuzi wanaona hofu hiyo inasababisha washindwe kujiamini katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kusababisha kutenguliwa au kuachwa wakati wa mabadiliko madogo.

“Kuna ile hali ya kujiuliza, hivi nikifanya uamuzi huu Rais atanichukuliaje,” alisema Profesa Mohamed Bakari, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyejikita katika sayansi ya jamii.

“Na tatizo linaanzia kwenye staili ya uongozi ya Rais mwenyewe unaotaka mabadiliko katika baadhi ya mambo. Unapokosa hali ya kujiamini, ubunifu pia unakosekana. Hata kama utateua wataalamu wazuri wenye profession (taaluma) zao.”

Mwingine aliyekubaliana na hoja hiyo ni Dk Abel Kinyondo wa taasisi ya utafiti ya Repoa, aliyesema pamoja na hofu, hali ya kukosa mamlaka juu ya baadhi ya mambo pia huchangia mawaziri kutoweza kutekeleza maamuzi yao ipasavyo au kutojiamini kuingilia kati migogoro kwa lengo la kuitatua.

“Juzi katika sakata la korosho, Rais aliagiza fedha na watu wa kusomba korosho wakapatikana,” alisema mtaalamu huyo wa utafiti.

“Lakini si rahisi kwa waziri. Na kinachosikitisha fedha hazipatikani kwa wakati na haziwafikii zote, hivyo waziri kufanya uamuzi unaohitaji rasilimali fedha na watu, humuwia vigumu kuuchukua.”

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hali ya sintofahamu inayosababisha kutojiamini kwa baadhi ya mawaziri inatokana na matukio tofauti.

Februari 21, akitokea nchini Uganda, Rais Magufuli alitengua uamuzi uliotolewa Januari na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyeagiza nyumba za kaya 1,900 zilizovamia eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza zibomolewe.

Rais Magufuli alitaka wasiendeleze makazi na kwamba Serikali haiwezi kukimbilia kuziondoa kaya hizo na badala yake itaangalia njia bora ya kufanya. Lukuvi hakuvuliwa uwaziri.

Mwingine aliyekumbana na hali hiyo ni Nape Nnauye, ambaye aliunda kamati ya kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa studio za kituo cha televisheni cha Clouds Media lililomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Wakati akijiandaa kuwasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Waziri Mkuu, kulifanyika mabadiliko madogo yaliyosababisha apoteze nafasi yake ya waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Akiwa Bandari ya Dar es Salaam ambako alifanya ziara ya kushtukiza, Rais alishangazwa kukuta magari yapatayo 53 ambayo mmiliki wake hakujulikana, akishangaa jinsi Dk Phillip Mpango ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango, na Profesa Makame Mbarawa walivyoshindwa kuwajibika.

Hata hivyo, mawaziri hao waliepuka kutenguliwa.

Pia amri ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kutaka wananchi wanaokutwa sokoni wakiuza samaki waliovuliwa kwa njia haramu, wasibughuziwe, ilitenguliwa na Rais aliyetaka wawajibishwe na kuonyesha walikopata samaki hao.