Jafo ahoji mradi wa stendi ya Mbezi Dar, atoa siku saba

Muktasari:

Kutokana na mradi wa stendi ya mabasi ya Mbezi Luis jijini Dar es Salaam kusuasua, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo ametoa siku saba wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kumpa taarifa za mradi husika


Dar es Salaam.  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo ametoa siku saba kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kumpa taarifa za juu maendeleo ya mradi wa stendi ya mabasi ya Mbezi- Luis jijini humo.

Amesema kinyume na hapo fedha zilizotengwa kiasi cha Sh50.9bilioni  zitaondolewa na kutumika katika miradi mingine kwa kuwa Serikali haifurahishwi na mwenendo wa mradi huo.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 13, 2018 jijini Dar es Salaam.

Pia, ameagiza Wilaya zilizopewa fedha za ujenzi wa hospitali na  hadi sasa hazijaanza ujenzi kufanya hivyo kabla ya Desemba 19, 2018 na zikishindwa, fedha zitachukuliwa.

“Ikifika Desemba 19, 2018 wilaya yoyote itakayokuwa haijaanza mchakato wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya na tayari imepewa fedha, zitachukuliwa na kupelekwa kwenye wilaya nyingine ambazo hazikupata fedha,” amesema.

“Nafahamu wazi kuna halmashauri mpaka leo hii watu wanalumbana wapi  hospitali ya wilaya ikajengwe wakati wananchi wanakosa huduma. Jambo hili linatuhuzunisha sana.”

Amesema ujenzi katika hospitali hizo unatakiwa uwe umekamilika kwa asilimia miamoja  ifikapo Juni 30, 2019.