Jaji Mkuu Tanzania asema Kiingereza kinawapiga chenga mawakili

Muktasari:

Wakati mawakili wapya 909 wakihitimu na kuingizwa kwenye orodha ya mawakili wa Mahakama Kuu, lugha ya Kiswahili imetajwa kuwa changamoto kwa wengi wao.


Dar es Salaam. Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma  amesema lugha ya Kiingereza kwa mawakili nchini Tanzania bado ni changamoto.

Amewataka mawakili wapya kujiendeleza kielimu kwa kutumia mitandao ili waendane na mabadiliko.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 14, 2018 katika mahafali ya 59 ya Shule Kuu ya Sheria kwa Vitendo ambako mawakili wapya 909 wamehitimu.

Profesa Juma amesema pamoja na kuwa mawakili hao wamepita safari ndefu ya masomo, bado ufanisi katika kujieleza kwa lugha ya Kiingereza upo chini.

Mahafali hiyo imehudhuriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Adelardus Kalangi, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Fatma Karume, mawakili na majaji wastaafu.

Amesema katika kuhimili ushindani,  kufahamu lugha ya Kiingereza kwa wanataaluma wa kada hiyo ni jambo lisilokwepeka na kuwataka mawakili kuendelea kujinoa.

"Binafsi nilipata nafasi adhimu sana kwa mujibu wa kifungu cha 8(3) cha  Sheria ya Mawakili kukutana ana kwa ana  na kila mmoja wenu kinachomtaka Jaji Mkuu ajiridhishe kama wakili mtarajiwa ana sifa stahiki," amesema.

Amesema pamoja na kupima uelewa wa masuala ya sheria, aliwapima uelewa wa matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza.

 "Niseme kuwa ufasaha katika kujieleza kwa lugha ya Kiingereza ni changamoto inayotakiwa kufanyiwa kazi au uongo? “ amehoji na kuibua vicheko miongoni mwa wahitimu.

Amewakumbusha mawakili kusimamia haki na maadili ya taaluma katika kutekeleza majukumu yao ili kuisaidia mahakama kufanya uamuzi wa haki.

Dk Kalangi amewataka mawakili kujiandaa kuitumikia jamii yao kwa kuepuka kugeuza taaluma hiyo kama njia ya kujitajirisha.