Jamii yamrudishia furaha mwanamke aliyetobolewa macho

Muktasari:

  • Juhudi mbalim-bali zimeendelea kufanyika iki-wamo kumfungulia akaunti ya benki ambayo tayari ina Sh1,100,000 ili anze kujengewa nyumba huku Serikali ikiahidi kuwarudisha shuleni watoto wake walio-katisha masomo.

“Sina cha kuwalipa Mungu ndiye anayejua wema mlionifanyia. Natamani kuona ili angalau nizione sura zenu. Nilikata tamaa nikaamini nitakufa na maisha magumu, lakini Mungu amekuleteni kwangu ili mnisaidie,” anasema Fatuma Maganga baada ya Mwananchi kufika nyumbani kwake kwa mara ya pili mwishoni mwa wiki iliyopita.

Jina la Fatuma Maganga (50) ambaye mwaka 2014 alibakwa kisha kutobolewa macho na Manyanda Mchenya anayetumikia kifungo cha miaka 17 gerezani, limevuta hisia za watu wengi hasa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Makundi mbalimbali ya kijamii yanafika nyumbani kwake baada ya tukio hilo kuripotiwa katika gazeti la Mwananchi, Novemba 13, mwaka huu.

Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji wa Kahama, Abdulrahman Nuru, anasema mchakato umefanyika kuhakikisha mwanamke huyo anasaidiwa.

Fatuma mwenyewe anasema tangu taarifa zake ziliposikika anashuhudia mabadiliko mbalimbali ikiwamo kutembelewa na makundi ya watu nyumbani kwake huku baadhi yao wakitaka kujua zaidi kuhusu mkasa huo uliompa ulemavu wa macho na kukimbiwa na mume wake Vicent Nkwabi.

“Nilikata tamaa ya maisha, lakini sasa naona ni kama miujiza inanitokea jinsi watu wanavyofika kila siku nyumbani kwangu na kutoa misaada mbalimbali yakiwamo mavazi, chakula na malazi. Nilikuwa nikilala chini na watoto wangu kwa kutandika viroba, lakini tayari nimenunuliwa kitanda, godoro, shuka na chandarua. Japokuwa sivioni lakini nalala vizuri,” anasema Fatuma

Anasema “Kama sio Mungu kutenda miujiza kwa kuileta Mwananchi kuchukua na kuandika taarifa za maisha yangu na wanangu 10 niliotelekezwa nao na mume wangu, matumaini yalikuwa yametoweka. Tulikuwa tukishindia kisamvu, lakini sasa tunakunywa mpaka chai na tayari wasamalia wema wananijengea nyumba. Nawashukuru wote wanaojitolea kunisaidia”.

Kwa mujibu wa Nuru, watumishi wa halmashuri ya Kahama walifika nyumbani kwa Fatuma na kumnunulia kitanda, magodoro, shuka na chandarua baada ya kushuhudia akilala chini.

Anasema mbali na msaada huo, pia walimkabidhi Sh600,000.

Marcelina Saulo ambaye ni Katibu wa TCCIA Mkoa wa Shinyanga, akiambata na wajasiriamali walifika kumjulia hali Fatuma na kusema wameguswa na maisha yake.

Anasema walikabidhi msaada wa chakula ukiwamo unga wa sembe, maharage, dagaa, chumvi na nguo kwa ajili yake na wanawe na kupitisha mchango ili kumjengea nyumba.

Marcelina anasema mbali na misada hiyo, pia walitoa Sh120,000 zimsaidie kwa mahitaji madogomadogo.

Hata hivyo, alizitupia lawama taasisi za serikali zinazohusika na huduma za jamii kutojua tukio la mama huyo ikiwa ni miaka minne sasa imepita.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Polisi Kahama, Minaeli Kisagase anasema wamefika kwa Fatuma zaidi ya mara moja na kuzungumza naye.

Mbali na hatua hiyo, anasema wamezunguka kwenye shule za msingi na sekondari kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwani tukio lililomkuta Fatuma halijawahi kutokea tangu aanze kufanya kazi kwenye dawati hilo.

Ofisa Elimu Kahama, Aluko Lukolela anasema ofisi yake itasimama imara kuhakikisha watoto wa mama huyo ambao wanastahili kuwa shuleni wanapata fursa hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba anasema, analiangalia suala hilo kisheria ili kukata rufaa nje ya muda kupinga hukumu iliyotolewa kwa mbakaji aliyefungwa miaka 17 ambapo anaungwa mkono na Minaeli aliyeahidi kutoa ushirikiano akisema mtu huyo alistahili kifungo cha maisha au miaka 30 jela.

Mume wa Fatuma aliwahi kuzungumza na Mwananchi na kusema alilazimika kuiacha familia yake kwa kuwa hana uwezo wa kuihudumia.