Jeshi la Magereza lazindua dawati jinsia

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua dawati la jinsia na mtandao wa askari wanawake wa Jeshi la Magereza na kuwataka askari hao wanawake kutobweteka na kusubiri kubebwa na badala yake wachape kazi

Dar es Salaam. Jeshi la Magereza nchini Tanzania  limezindua dawati la jinsia na mtandao wa askari wake wanawake kwa lengo la kushughulikia masuala ya jinsia na kuleta usawa katika fursa.

Pia,  limezindua sera ya haki na ulinzi wa watoto wanaokuwa gerezani.

Akizungumza leo Ijumaa Desemba 7, 2018 katika uzinduzi huo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema uwapo wa dawati hilo ni ishara kwamba Jeshi la Magereza  limeamua kwa dhati kuweka mkazo masuala ya usawa wa kijinsia.

Ametumia fursa hiyo kuwataka askari wa kike kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa zinazojitokeza na sio kusubiri kubebwa.

“Tatizo tulilonalo baadhi ya wanawake ni kutojituma tukisubiri kuwezeshwa.  Sasa fursa hii ya dawati ikawe chachu mkaonyeshe uwezo wenu ili hata zinapotokea fursa isiwe inaonekana kuna upandeleo,” amesema Ummy.

Awali,  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,  Hamad Masauni alieleza kuwa Magereza kuanzisha dawati na mtandao huo kunaenda kutatua changamoto zinazohusu mambo ya kijinsia ikiwamo kukosekana kwa fursa sawa za uongozi.

Amesema wizara yake itafanya kila linalowezekana kulinda haki za wanawake na watoto waliopo magerezani.