Kada CCM ajitosa urais 2020

Muktasari:

Wanachama 38 wa CCM walichukua fomu kuomba kupitishwa kugombea urais mwaka 2015, lakini chama hicho kilim-pitisha Rais John Magufuli.

Tanga. Kada wa CCM, ambaye mwaka 2015 alijitosa kuwania kupitishwa na chama hicho kuwania urais, Dk Muzzammil Kalokola ana mpango wa kuingia tena kwenye mbio hizo mwaka 2020, na hivyo kuwa mpinzani wa kwanza wa Rais John Magufuli.

CCM ina utaratibu wa kumuachia mshindi wa urais katika uchaguzi, atetee kiti chake kuhitimisha awamu mbili za miaka mitano kila moja, lakini Dk Kalokola ataweka changamoto katika utamaduni huo.

“CCM tulijiwekea utaratibu wa kumuachia Rais kuwa mgombea pekee pale anapomaliza miaka mitano ili akamilishe mitano mingine ili kipindi chake cha miaka 10 kikamilike,” alisema Dk Kalokola katika mazungumza maalum na Mwananchi.

“Lakini Rais Magufuli amekiuka misingi kwa hivyo hakuna sababu ya kumwachia. Kwa hiyo nitaomba ridhaa nipitishwe.”

Dk Kalokola, mchumi anayeongoza asasi ya Mwalimu Nyerere Ideology Conservation Society, amedai kuwa Rais John Magufuli amekiuka misingi ya CCM kwa kuwapa nafasi za uongozi wapinzani wa chama hicho wanaojiunga na chama hicho tawala.

Kitendo hicho kinawavunja nguvu wanachama waliopigania kuiweka CCM madarakani, alisema Dk Kalokola ambaye aliwahi kufungua kesi dhidi ya Serikali akipinga uteuzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na posho alizosema ni mzigo kwa Taifa.

Alisema ndani ya CCM kuna hazina kubwa ya watu wenye uadilifu na uzalendo usiotiliwa shaka na ambao kama Rais Magufuli angewatumia wangeweza kumsaidia kuendesha nchi kutokana na uzoefu wao katika uongozi, lakini anawaacha na badala yake anawachukua wanaotoka upinzani.

“Haiwezekani mtu ambaye wakati wa kampeni za kuwania urais mwaka 2015 alikuwa akimtukana na kutumia njia zote kuhakikisha Magufuli anakosa urais, leo ametangaza kuingia CCM, kesho jina lake linapitishwa kugombea ubunge, keshokutwa anakuwa waziri,” alisema Dk Kalokola.

Hata hivyo, alimsifu Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi.

Alimshauri Rais awe anawateua hata waliogombea urais 2015 kwa sababu kila mmoja ana uzoefu wake.

Alitoa mfano wa Jaji Augustino Ramadhani ambaye amebobea katika masuala ya sheria na anaheshimika Afrika na duniani; aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Mohammed Ghalib Bilal na pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akisema wangemsaidia katika utendaji.

“Sisi wengine ni wataalamu wa uchumi, tunafahamu wapi tulikotoka na wapi tulikosea,” alisema Dk Kalokola, ambaye taasisi yake inajihusisha na kuhifadhi mawazo ya Mwalimu Nyerere.

“Kuna wakati (Nyerere) alisema ukigeuka nyuma utageuka jiwe, kosa linalofanyika ni kuwakabidhi rasilimali na biashara wageni, sisi tunabaki na uhuru wa bendera peke yake.”

Tayari katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali yuko kwenye mgogoro na waziri wa zamani, Bernard Membe akimtuhumu kuanza mikakati ya kugombea urais 2020. Lakini Dk Kalokola amekwenda mbali zaidi kwa kutangaza nia, hali inayoweza kusababisha aadhibiwe.