Kakunda: Usajili wa vikundi vya kijasiriamali usiwe na ubaguzi

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda

Muktasari:

  • Serikali imewataka maofisa maendeleo ya jamii katika halmashauri zote nchini kutowabagua watu kwa kigezo cha mkoa wanaozaliwa wakati wa usajili wa vikundi vya kijasiriamali.

Mtwara. Kutokana na baadhi ya maofisa  maendeleo ya jamii kubagua watu wanaoomba kusajiliwa kama kikundi kumesababisha baadhi ya vikundi kubadili majina ya watu ili kukidhi mahitaji ya msajili.

Hayo yameelezwa leo na mmoja wa wabanguaji wadogo wa korosho ambaye amedai wakati wa kuomba usajili walidaiwa siyo wakazi wa eneo husika ambalo walitaka kufanyia shughuli zao za ubanguaji kutokana na majina yao.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichoitishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mmoja wa wabanguaji, John Joseph  amesema kutokana na ubaguzi huo alilazimika kuondoa baadhi ya majina ya watu na kuweka ambao hawakuwa na ndoto sawa.

 “Mnapotengeneza kikundi mnaandaa ninyi  muundo wa kikundi , uongozi na mfanye nini lakini athari iliyonikuta ilibidi tubadili uongozi na watu wengine tuwatoe na kuweka watu ambao hata hawajui ndoto yetu ni ipi na makusudi yetu ni yapi, cha msingi tukidhi mahitaji ya msajili,” amesema Joseph.

Kufuatia madai hayo,  Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda ametoa agizo kwenda kwa maofisa maendeleo ya jamii wote katika halmashauri zote nchini kuwa hawatakiwi na sheria kubagua Mtanzania yeyote kwa kuangalia alipotoka.

 “Hata kama ametoka Bukoba, ametoka Mara , Shinyanga anaishi Mtwara huwezi kusema eti hatukusajili wewe kama kikundi kwa sababu siyo mtu wa huku , akijulikana ofisa maendeleo ya jamii aliyefanya hivyo tupeni majina yake ili aweze kufanyiwa kazi na Serikali, Watanzania hawatakiwi kubaguliwa ,” amesema Kakunda.